Lebo

10/12/2014

ASOMAYE NA AFAHAM



"Danieli aliazimu moyoni mwake ya kuwa hatajitia unajisi
kwa chakula cha mfalme, wala kwa divai aliyokunywa; basi
akamwomba yule mkuu wa matowashi ampe ruhusa asijitie unajisi"
(Dan. 1:8). Ni ujasiri ulioje! Ombi lake halikuwa rahisi
kukubaliwa na msimamizi yule kwa vile angekatwa kichwa kama
wangeonekana wamekondeana (Dan. 1:10). Basi Danieli akamwambia,

"Tafadhali utujaribu sisi watumishi wako muda wa siku kumi; na
watupe mtama [nafaka, kokwa, mboga za majani, matunda] tule, na
maji tunywe. Kisha nyuso zetu zitazamwe mbele yako, na nyuso za
wale vijana wanaokula chakula cha mfalme..." (Dan. 1:13).
Akawakubalia ombi hilo.

Je! mambo yalikuwaje kiafya baada ya
siku zile kumi tu? "Nyuso zao zilikuwa nzuri zaidi [wanawake
wanaohangaika na vipodozi vinavyodhuru afya wangezingatia hilo],
na miili yao ilikuwa imenenepa zaidi, kuliko wale vijana wote
waliokula chakula cha mfalme. Basi yule msimamizi akaiondoa
posho yao ya chakula [cha mfalme], na ile divai waliyopewa
wanywe, akawapa mtama [nafaka, kokwa, mboga za majani, matunda] tu" (Dan. 1:15,16).

Chakula cha matajiri au wafalme tunachokitamani sana
hakileti afya mwilini. Chakula rahisi cha mimea na maji safi na
salama ni lishe bora. Kwa akili safi na mwili wenye afya,
ulionenepa kiafya sio kwa ugonjwa, tumia vyakula vya mimea na
maji safi na salama, na kufuata Kanuni zile 8 za Afya. Wanasayansi wamegundua kuwa wale wanaokula vyakula vya mimea bilanyama wanaishi maisha marefu sana kuliko wanaokula nyama Danieli naye aliishi zaidi ya miaka 80 kufikia kipindi cha utawala wa Koreshi (Dan. 1:21; 10:1)

Hebu tuwafuatilie vijana wale wanne mwisho wa mafunzo yao ya miaka mitatu. Mfalme Nebukadreza aliwaonaje?
"Naye mfalme akazungumza nao; na miongoni mwao wote
hawakuonekana waliokuwa kama Danieli, na Hanania, na Mishaeli,
na Azaria... Na katika kila jambo la hekima na ufahamu
alilowauliza mfalme, akawaona kuwa wanafaa mara kumi zaidi ya
waganga na wachawi waliokuwa katika ufalme wake" (Dan.1:19,20).

Kwa nini tuhangaike sana na suala la afya ya mwili wetu,
je! maisha ya kiroho si bora zaidi? "Mpenzi naomba ufanikiwe
katika mambo yote na kuwa na afya yako [kimwili], kama vile roho
yako ifanikiwavyo" (3 Yohana 2).

Wahenga walisema,

"Akilitimamu katika mwili wenye afya." Ni shauri la kuzingatiwa sana.
Kanuni ya Biblia ni hii: "

Basi, mlapo, mnywapo, au mtendapo
neno lo lote fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu" (1 Kor. 10:31).
Tunawajibika kuitunza miili yetu katika hali ya afya nzuri
kadiri iwezekanavyo (l Kor. 6:19,20; 1 Pet. 1:18,19;
Rum.12:1,2).

Suala la afya linahusu wokovu wetu. Mungu anaweza
kututumia kama Danieli (Dan. 1:17).