Lebo

29/11/2016

Kujifunza Kuomba Maombi ya Kweli

SEHEMU YA KWANZA



MUNGU huzungumza nasi kupitia katika viumbe vyake vya asili na mafunuo yake, kupitia katika maongozi yake, na kwa njia ya Roho wake. Lakini njia hizo hazitoshi; sisi pia tunahitaji kumfungulia mioyo yetu. Ili tupate uzima wa kiroho na nguvu yake, hatuna budi kuongea na Baba yetu aliye mbinguni. Mawazo yetu yanaweza kuvutwa kwake; tunaweza kuzitafakari kazi zake, rehema zake, baraka zake; lakini hayo, kwa maana yake kamili, si kuongea naye. Ili tuweze kuongea na Mungu, ni sharti tuwe na mambo fulani ya kumwambia hasa kuhusu maisha yetu tunayoishi.Katika kuomba tunamfunulia Mungu mioyo yetu na kuongea naye kama tunavyoongea na rafiki wa kweli. Si lazima kufanya hivyo ili kumjulisha Mungu hali yetu ilivyo, bali kuongea naye kunatuwezesha kumpokea mioyoni mwetu.

Maombi hayamlazimishi Mungu kushuka kwetu, bali ni sisi ambao tunainuliwa mpaka kufika
kwake. Yesu alipokuwapo hapa duniani, aliwafundisha wanafunzi wake kusali. Aliwaagiza waweke mahitaji yao ya kila siku mbele za Mungu, na kumtwika mizigo yao yote. Na ahadi ile aliyowapa kwamba dua zao zingesikilizwa ni ahadi iliyotolewa kwetu pia. Yesu mwenyewe, alipokaa na wanadamu, aliomba mara nyingi.
Mwokozi wetu alishiriki katika shida zetu na udhaifu wetu; hivyo akawa mhitaji na mwombaji, akimwomba Baba yake ili apate nguvu mpya za kufanya kazi yake na kuwa tayari kupambana na kazi na majaribu yatakayompata. Yeye ndiye mfano wetu katika mambo yote. Ni ndugu yetu ashirikiye udhaifu wetu, “alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote;” lakini kwa sababu alikuwa hana dhambi, aliyaepuka maovu nafsini mwake; alistahimili mapambano na maumivu makali moyoni mwake katika dunia hii yenye dhambi. Ubinadamu wake ulifanya maombi kuwa ya lazima kwake na haki yake.

Alipata faraja na furaha katika kuongea na Baba yake. Na iwapo Mwokozi huyo wa wanadamu, Mwana wa Mungu, aliona kwamba anahitaji kuomba, je! sisi, tulio wanadamu dhaifu wenye dhambi, tusingeona kwamba ni jambo la lazima zaidi kwetu kuomba bila kukoma. Baba yetu aliye mbinguni anangojea kutumwagia baraka zake juu yetu kwa utimilifu. Ni fursa yetu kunywa maji mengi kwenye chemchemi ya pendo lake.
Ni jambo la kushangaza jinsi gani ya kwamba sisi tunaomba kidogo mno! Mungu yu tayari, tena
anapenda kusikiliza maombi ya kweli ya mtoto wake aliye duni kabisa, walakini sisi kwa upande wetu hatuna moyo sana wa kumwambia Mungu haja zetu. Hivi malaika wa mbinguni wanafikirije kuhusu wanadamu maskini wasio na msaada wo wote, ambao wanakabiliwa na majaribu, wakati moyo wa Mungu uliojaa upendo usio na kikomo unapowaonea shauku nyingi sana, akiwa tayari kuwapa zaidi ya yale waombayo au kufikiria, na bado maombi yao ni kidogo sana, tena wana imani ndogo kabisa? Malaika wanapenda kusujudu mbele zake Mungu; wanapenda kuwa karibu naye. Wanaona kwamba maongezi yao na Mungu ni upeo wa furaha yao; lakini watoto wa dunia hii,
wanaohitaji msaada mwingi mno ambao ni Mungu pekee awezaye kuwapa, wanaonekana
kana kwamba wametosheka kutembea bila ya kuwa na nuru ya Roho wake, yaani, ushirika wa kuwako kwake.

Giza la Shetani huwafunika wale wanaoacha kuomba. Majaribu ya adui huyo anayonong’ona masikioni mwao huwashawishi wafanye dhambi; na hayo yote ni kwa sababu wao hawazitumii haki zote alizowapa Mungu katika mpango wa mbinguni wa maombi aliowawekea. Kwa nini wana na binti zake Mungu ni wazito sana kuomba, wakati maombi ni ufunguo katika mkono wa imani uifunguao ghala ya mbinguni, ambamo zimewekwa hazina za msaada na mibaraka isiyo na mwisho ya Mungu mwenye uweza wote? Tusipoomba bila kukoma na kukesha kwa bidii, tutakuwa katika hatari ya kutojali na kukengeuka kutoka katika njia ile ya haki. Adui hutafuta daima kuzuia njia iendayo kwenye kiti cha rehema, ili kwa maombi ya dhati na imani tusiweze kupokea
neema na nguvu ya kutusaidia kuyapinga majaribu.

KUMJUA MUNGU

SOMO LA TATU.



Tusifungue kabisa Biblia na kuyasoma maneno yake bila kuomba. Kabla ya kuzifungua kurasa zake ingetupasa kuomba ufahamu kutoka kwa Roho Mtakatifu, naye atatupa. Nathanaeli alipomwendea Yesu, Mwokozi alisema, “Tazama, Mwisraeli kweli kweli, hamna hila ndani yake.” Nathanaeli akamwambia, “Umepataje kunitambua?”Yesu akajibu, akamwambia, “Kabla Filipo hajakuita, ulipokuwapo chini ya mtini, nilikuona.” Yoh. 1:47,48. Na Yesu atatuona sisi mahali pa siri pa sala, ikiwa tutamwomba ili tupate kuelimishwa na kuyajua yaliyo ya kweli.

Malaika watokao kwenye ulimwengu ule wa nuru watakuwa pamoja na wale ambao kwa unyenyekevu wa moyo wanatafuta uongozi wa Mungu. Roho Mtakatifu humwinua na kumtukuza Mwokozi. Ni kazi yake kutuonyesha Kristo, na hali yake jinsi ilivyo yenye haki na usafi, na kutudhihirishia habari za wokovu mkuu tupatao kwake. Yesu alisema, “Atatwaa katika yaliyo yangu, na kuwapasha habari.” Yohana 16:14. Roho wa kweli ndiye mwalimu pekee awezaye kutujulisha
barabara ile kweli ya Mungu. Ni dhahiri kwamba Mungu huwaona wanadamu kuwa wa thamani kubwa, kwa kuwa alimtoa Mwanawe afe kwa ajili yao, tena amemweka Roho
wake kuwa mwalimu na kiongozi wa wanadamu daima.
               

Nataka nimjue Yesu,
Na nizidi kumfahamu;
Nijue pendo lake tu,
Wokovu wake kamili.

Nataka nione Yesu,
Na nizidi kusikia
Anenapo kitabuni,
Kujidhihirisha kwangu.

Nataka tena zaidi,
Daima kupambanua
Mapenzi yake, nifanye
Yale yanayompendeza.

Nataka nikae naye,
Kwa mazungumzo matamu.
Nizidi kuwaonyesha
Wengine wokovu wake.

Zaidi, zaidi,
Nimfahamu Yesu,
Nijue upendo wake,
Wokovu wake kamili.