Lebo

02/12/2016

Kujifunza Kuomba Maombi ya Kweli

SEHEMU YA TATU.


Tunapomwendea Mungu kumwomba rehema zake na mbaraka wake, ingetupasa kuwa na roho ya upendo ndani ya mioyo yetu wenyewe. Twawezaje kuomba hivi, “Utusamehe deni zetu, kama sisi nasi tuwasamehevyo wadeni wetu,” wakati sisi katika roho zetu tungali hatujakubali kuwasamehe wengine. Tukitumaini kujibiwa maombi yetu, sharti tuwe na roho ya kuwasamehe wengine kwa njia ile ile, na kwa kiwango kile kile, kama sisi tunavyotarajia kusamehewa.

Kudumu katika maombi ni sharti jingine lililowekwa ili tupate kupokea.Yatupasa kuomba sikuzote, kama tunataka kukua katika imani na katika uzoefu wa maisha yetu. “Katika kusali, mkidumu,” “dumuni sana katika kuomba, mkikesha katika kuomba huku na shukrani.” Rum. 12:12; Kol. 4:2. Petro awausia Wakristo, “Iweni na akili, mkeshe katika sala.” 1 Petro 4:7. Mtume Paulo awaagiza hivi, “Katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane kwa Mungu.” Flp.4:6. Na Yuda pia asema, “Ninyi, wapenzi, mkijijenga juu ya imani yenu iliyo takatifu
sana, na kuomba katika Roho Mtakatifu, jilindeni katika upendo wa Mungu.” Yuda 20,21. Kuomba bila kukoma ni muungano wa mtu na Mungu usioweza kuvunjika, kiasi kwamba uhai toka kwa Mungu unabubujika na kuingia katika maisha yetu; na kutoka katika maisha yetu usafi wa maisha na utakatifu hububujika na kumrudia Mungu.

Umuhimu upo wa kufanya bidii katika kuomba; usikubali kitu cho chote kikuzuie kuomba fanya kila jitihada kuacha wazi mawasiliano kati ya roho yako na Yesu tafuta kila nafasi kwenda mahali ambapo watu huzoea kuomba wale wanaotaka kushirikiana na Mungu kweli kweli wataonekana kila mara kwenye mkutano wa maombi; watakuwa waaminifu katika kufanya wajibu wao, tena watakuwa na bidii na shauku katika kujipatia manufaa yote wawezayo kupata. Watatumia vizuri kila nafasi wapatayo ili kujiweka mahali wawezapo kupokea mionzi ya nuru kutoka mbinguni.

Sharti tuombe pamoja na watu wa nyumbani; na zaidi ya yote tusiwe wavivu katika kuomba faraghani peke yetu; maana kufanya hivyo ndiyo asili ya uzima wa roho zetu. Ni vigumu kabisa kusitawi kiroho wakati maombi yanapuuzwa. Maombi pamoja na watu wa nyumbani na yale ya watu wengi katika ibada hayatoshi. Hebu mahali pale pa faragha moyo wako na ufunguliwe wazi ili upate kuchunguzwa na jicho lake Mungu.
Maombi ya faragha ya mtu akiwa peke yake yanapaswa kusikilizwa tu na Mungu asikiaye maombi. Hakuna sikio lo lote lenye udadisi linalopaswa kupokea mzigo wa dua kama hizo. Katika maombi hayo ya siri mtu hasumbuliwi na mivuto inayomzunguka, hasumbuliwi na misisimko yo yote. Kwa utulivu, lakini kwa dhati, moyo wake unamtafuta Mungu. Mvuto utokao kwake yeye aonaye sirini, ambaye sikio lake li wazi kusikiliza maombi yatokayo moyoni, utakuwa mtamu na wa kudumu. Kwa imani tulivu, ya kawaida, mtu huyo anaongea na Mungu, na kujikusanyia mionzi ya nuru itokayo kwa Mungu inayomtia nguvu na kumtegemeza katika mapambano yake na Shetani. Mungu ni mnara wa nguvu zetu. Omba katika chumba chako cha siri; na unapokwenda kufanya kazi zako za kila siku, umwinulie Mungu moyo wako mara kwa mara. Hivyo ndivyo Henoko alivyopata kutembea pamoja na Mungu. Maombi hayo ya kimya kimya hupanda juu kama uvumba wa thamani kwenda mbele ya kiti cha neema. Shetani hawezi kamwe kumshinda yule ambaye moyo wake humtegemea Mungu hivyo.

Hakuna wakati wala mahali pasipofaa kumwomba Mungu. Hakuna kinachoweza kutuzuia tusimwinulie mioyo yetu tukiwa na roho ya maombi ya dhati. Tukiwa katika makundi ya watu mitaani, katikati ya shughuli zetu za kazi, tunaweza kupeleka dua zetu kwa Mungu, na kumwomba atupe uongozi wake, kama alivyoifanya Nehemia alipotoa ombi lake mbele ya Mfalme Artashasta. Chumba cha siri cha mawasiliano kinaweza kupatikana po pote tulipo. Mlango wa moyo wetu ungefunguliwa wazi daima, na mwaliko wetu ungepanda juu ili Yesu aje na kukaa ndani ya moyo wetu kama mgeni atokaye mbinguni.