Lebo

26/09/2016

KAZI NA MAISHA........

SOMO LA KWANZA


MUNGU ndiye asili ya uhai na mwanga na furaha kwa malimwengu yote. Kama mionzi ya nuru kutoka juani, kama vijito vya maji kutoka kwenye chemchemi hai, baraka zinamiminika kutoka kwake kwenda kwa viumbe vyake vyote. Na kila mahali ambapo uhai wa Mungu umo ndani ya mioyo ya wanadamu, utabubujika kuwa upendo na mbaraka kwa wengine.
Ilikuwa ni furaha ya Mwokozi wetu kuwainua na kuwakomboa wanadamu walioanguka dhambini. Kwa ajili hiyo hakuyahesabu maisha yake kuwa ni kitu cha thamani kwake, lakini “aliustahimili msalaba na kuidharau aibu.” Ebr. 12:2. Kwa ajili hiyo malaika wanashughulika daima katika kazi ya kuwaletea wengine furaha. Hiyo ndiyo furaha yao. Ile ambayo watu wale wajipendao binafsi wangeiona kuwa ni kazi ya kuwavunjia heshima, yaani, kuwahudumia wale walio na hali mbaya na ambao kwa kila hali ni duni kwa tabia na hadhi zao, ndiyo kazi waifanyayo malaika wasio na dhambi.Roho aliyo nayo Kristo ya upendo unaojitoa mhanga ndiyo roho iliyoenea kule mbinguni,
na ndiyo msingi hasa wa furaha kuu iliyoko kule. Hiyo ndiyo roho watakayokuwa nayo
wafuasi wake Kristo, ndiyo kazi watakayofanya.

Upendo wa Kristo ukiwamo moyoni, kama manukato yenye harufu nzuri, hauwezi kufichika. Mvuto wake mtakatifu utawagusa wote tunaokutana nao. Roho ya Kristo ikiwamo moyoni ni kama chemchemi jangwani, inayobubujika na kuwaburudisha wengi, na kuwafanya wale walio tayari kuangamia kutamani kunywa maji ya uzima. Kuwa na upendo kwa Yesu kutadhihirika kwa njia ya kuwa na tamaa ya kutenda kama alivyotenda yeye, kwa madhumuni ya kuwaletea furaha na kuwatia moyo wanadamu. Kutaleta upendo, upole, na huruma kwa viumbe vyote vya Baba yetu aliye mbinguni anayevitunza.
Maisha ya Mwokozi wetu alipokuwa hapa duniani hayakuwa maisha ya raha, wala ya kujishughulikia mwenyewe tu, lakini daima alijitahidi kufanya kazi kwa bidii, bila kuchoka kwa ajili ya wokovu wa wanadamu waliopotea. Tangu kuzaliwa kwake mpaka kusulibiwa kwake pale Kalwari, alifuata njia ya kujinyima, wala hakutaka aachiliwe asifanye kazi za sulubu, safari zenye kumletea maumivu, na shughuli kwa watu zinazochosha mno na kazi za kawaida. Alisema, “Kama vile Mwana wa Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.”
Mathayo 20:28. Hilo lilikuwa ndilo lengo moja kuu la maisha yake. Mambo mengine yote yalichukua nafasi ya pili na kulisaidia lengo hilo. Kilikuwa ni chakula na kinywaji chake kufanya mapenzi ya Mungu na kuimaliza kazi yake (Yoh. 4:34). Nafsi na umimi havikuwa na nafasi katika kazi yake.

Kwa hiyo wale wanaoshiriki neema ya Kristo watakuwa tayari kujinyima sana, ili wengine aliowafia wapate karama hiyo. Watafanya kila wawezalo kuifanya dunia hii iwe mahali pazuri kwa ajili ya kukaa kwao hapa. Roho hii ni matokeo ya hakika ya kukua kiroho kwa mtu yule aliyeongoka kweli kweli. Mara tu anapokuja kwa Kristo, ndani yake hujitokeza shauku ya kuwajulisha wengine jinsi alivyomwona Yesu kuwa rafiki wa thamani sana kwake; kweli ile iokoayo na kutakasa haiwezi kufungiwa moyoni mwake. Kama tumevikwa haki ya Kristo, na kujazwa furaha ya Roho wake akaaye ndani yetu hatutaweza kunyamaza. Kama tumeonja na kuona kwamba Bwana ni mwema, tutakuwa na jambo fulani la kusimulia. Kama Filipo alivyomwona Mwokozi, tutawaalika wengine
kuja mbele yake. Tutajitahidi kuweka mbele yao mambo ya kuvutia pamoja na mambo yale ya kweli ya ulimwengu ule ujao ili waje kwa Kristo. Tutakuwa na shauku kubwa kuifuata njia ile aliyokwenda Yesu. Tutatamani kwa dhati sana kwamba wale watuzungukao waweze kumwona “Mwana-Kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu.” Yoh. 1:29