Lebo

24/09/2016

KUKUA KATIKA KRISTO

SOMO LA TATU.





Kama mtu anajifikiria nafsi yake tu, roho yake hugeuka na kutoka kwa Kristo ambaye ni uwezo na uzima wake. Kwa hiyo ni juhudi ya Shetani ya kudumu kuyageuzia mbali na Mwokozi mawazo ya mtu, kwa njia hiyo kumzuia kuungana na kushirikiana na Kristo. Anasa za dunia, masumbufu ya maisha haya na mashaka na huzuni, makosa ya wengine, au makosa na upungufu wako mwenyewe - kwa mojawapo au yote hayo Shetani atayaelekeza mawazo ili kuyapotosha (Tazama Mathayo 14:30). Usidanganywe na hila zake. Wengi wanaotaka kufanya yapasayo na kujitoa maisha yao kwa Mungu,
mara nyingi huvutwa na Shetani kufikiri sana juu ya makosa yao na udhaifu wao wenyewe, na hivyo kwa kuwatenga mbali na Kristo anatumainia kuwashinda.
Tusifikirie nafsi zetu sana, na kuhangaika na kuogopa iwapo kweli tutaokolewa. Mambo hayo yote
huugeuzia mbali moyo kutoka kwa Kristo aliye Asili ya nguvu zetu. Weka roho yako mkononi mwa Mungu kama amana, na umtumainie yeye. Mazungumzo yako na fikara zako ziwe juu ya Yesu. Nafsi yako na ifichwe ndani yake. Tupilia mbali mashaka yako yote; ziondolee mbali hofu zako. Sema kama alivyosema mtume Paulo:“Nimesulibiwa pamoja na Kristo; lakini ni hai; wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu; na uhai nilio nao sasa katika mwili, ninao katika imani ya Mwana wa Mungu, ambaye alinipenda akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu. Gal. 2:20. Tulia ndani ya Mungu. Yeye aweza kukilinda kile ulichokiweka amana kwake. Kama unajiweka mkononi mwake,
atakuwezesha upate kushinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyekupenda. Soma Warumi 8:37.
Kristo alipoutwaa mwili wa kibinadamu, aliwafungia kwake wanadamu kwa

kifungo cha upendo wake kisichoweza kuvunjwa na uwezo wo wote, isipokuwa kwa chaguo la mwanadamu huyo mwenyewe. Shetani atajitahidi daima kutuletea vishawishi vyake ili kukivunjilia mbali kifungo hicho - yaani, kutufanya tuchague wenyewe kujitenga mbali na Kristo. Hapo ndipo tunapohitaji kuwa macho, kujitahidi, na kuomba ili tusishawishiwe na jambo lo lote kuchagua kutawaliwa na bwana mwingine; kwa maana sikuzote sisi tunao uhuru kufanya hivyo. Lakini hebu na tumkazie Kristo macho yetu, naye atatulinda. Tukimtazama Yesu, tutakuwa salama. Hakuna awezaye
kutupokonya katika mkono wake. Tukimwangalia Yesu daima, “tunabadilishwa tufanane na mfano uo huo, toka utukufu hata utukufu, kama vile kwa utukufu utokao kwa Bwana aliye Roho.” 2 Kor. 3:18.Hivyo ndivyo wanafunzi wake wa zamani walivyopata kufanana na Mwokozi wao waliyempenda. Wanafunzi wale walipoyasikia maneno ya Yesu, walijisikia kuwa wanamhitaji. Walimtafuta, wakamwona, na kumfuata. Walikuwa pamoja naye nyumbani, mezani, chumbani, na mashambani. Walikuwa pamoja naye kama wanafunzi wa shule wanavyokuwa pamoja na mwalimu wao, wakipokea kila siku mafundisho ya ile kweli takatifu kutoka kinywani mwake. Walimtegemea kama watumishi wanavyomtegemea bwana wao, ili wapate kujua wajibu wao.

Wanafunzi wale walikuwa ni wanadamu wenye “tabia moja na sisi.” Yak. 5:17. Walikuwa na pambano lile lile dhidi ya dhambi kama sisi. Waliihitaji neema ile ile ili wapate kuishi maisha matakatifu. Hata na Yohana, mwanafunzi mpendwa wa Yesu, aliyefanana naye kwa ukamilifu kuliko wale wengine, hakuzaliwa akiwa na tabia nzuri. Alikuwa si mtu aliyependa tu kuwa kimbelembele na kutaka heshima, bali alipoumizwa alikuwa mwenye harara na chuki moyoni mwake. Lakini tabia ya Yule Mtakatifu ilipofunuliwa kwake, aliona mapungufu yake mwenyewe, naye akanyenyekea kutokana na ujuzi ule alioupata. Aliona nguvu na uvumilivu, uwezo na huruma, utukufu na upole katika maisha ya kila siku ya yule Mwana wa Mungu, mambo hayo yaliujaza moyo wake na sifa na upendo. Siku kwa siku moyo wake ulizidi kuvutwa kwa Yesu Kristo. Mpaka akajisahau nafsi
yake mwenyewe kutokana na upendo aliokuwa nao kwa Bwana wake, tabia yake ya harara na kutaka makuu ikashindwa chini ya uwezo wa Kristo ubadilishao tabia.
Uwezo wa Roho Mtakatifu ufanyao tabia ya mtu kuwa mpya uliufanya moyo wake kuwa mpya. Nguvu ya upendo wake Kristo ilifanya badiliko kamili la tabia yake. Hayo ndiyo matokeo ya hakika kwa mtu ye yote anayeunganika na Yesu. Kristo akaapo moyoni, tabia yote hubadilika kabisa. Roho wake Kristo, upendo wake, huulainisha moyo, na kuitawala nafsi ya mtu, na kuyainua juu mawazo yake na tamaa zake kuelekea kwa Mungu na mambo ya mbinguni. Yesu alipopaa kwenda mbinguni, wafuasi wake bado walikuwa na hisia ya kuwapo kwake. Kulikuwa ni kuwapo kwake kimwili, akiwa amejaa upendo na nuru.
Yesu, Mwokozi, aliyekuwa ametembea na kuongea na kuomba pamoja nao, aliyekuwa amesema maneno yenye tumaini na faraja mioyoni mwao, wakati ujumbe huo wa amani
ulipokuwa bado unatoka kinywani mwake, alikuwa amechukuliwa kwenda juu mbinguni, na sauti hii ya maneno yake ilikuwa imekuja kwao tena, wakati lile wingu la malaika lilipompokea – “Tazama, mimi nipo pamoja nanyi sikuzote, hata ukamilifu wa dahari.” Mathayo 28:20. Alikuwa amepaa kwenda mbinguni akiwa na mwili wa kibinadamu. Walijua kwamba yuko mbele ya kiti cha enzi cha Mungu, akiwa bado ni Rafiki yao na Mwokozi wao; na kwamba huruma yake ilikuwa haijabadilika; na kwamba yeye bado alikuwa amejifungamanisha na wanadamu wanaoteseka. Alikuwa akionyesha mbele za Baba yake sifa za damu yake ya thamani, akimwonyesha mikono yake na miguu yake
iliyojeruhiwa, kukumbuka gharama aliyokuwa amelipa kwa ajili ya watu wake waliokombolewa. Walijua kwamba alikuwa amepaa kwenda mbinguni kuwaandalia mahali, na ya kwamba atakuja tena, na kuwachukua kwenda nao kwake. Walipokutana, baada ya kupaa kwake, walikuwa na hamu ya kupeleka maombi yao kwa Baba kwa jina la Yesu. Kwa kicho kikuu waliinamisha vichwa vyao chini
walipoomba, wakarudia kusema ahadi yake hii, “Mkimwomba Baba neno lo lote atawapa
kwa jina langu. Hata sasa hamkuomba neno kwa jina langu, ombeni, nanyi mtapata; furaha yenu iwe timilifu.” Yoh. 16:23,24. Waliunyosha mkono wao wa imani juu zaidi na juu zaidi, wakiwa na hoja hii yenye nguvu, “Kristo ndiye aliyekufa; naam, na zaidi yahayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea.” Warumi 8:34. Na siku ya Pentekoste wakapata kujazwa Roho Mtakatifu, yule Mfariji ambaye Kristo alisema juu yake, “Naye atakuwa ndani yenu.” Naye alikuwa ameongeza kusema, “Yawafaa ninyi mimi niondoke; kwa maana mimi
nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu; bali mimi nikienda zangu, nitampeleka kwenu.” Yoh. 14:17; 16:7. Tangu siku hiyo, kwa njia ya Roho Mtakatifu, Kristo hukaa mioyoni mwa watu wake sikuzote. Muungano wao pamoja naye ulikuwa wa karibu sana kuliko wakati alipokuwa pamoja nao kimwili. Nuru, na upendo, na uweza wa Kristo akaaye ndani yao uliangaza nje kupitia kwao, hata watu walipowatazama “wakastaajabu, wakatambua ya kwamba walikuwa pamoja na Yesu.” Matendo 4:13.