Sehemu ya 2
Hatutaikataa dhambi mpaka hapo tutakapoona ubaya wake ulivyo hasa; yaani ,hapatakuwa na
badiliko la kweli katika maisha yetu mpaka hapo tutakapogeuka katika mioyo yetu na kwenda mbali nayo,Kuna watu wengi wanaoshindwa kuelewa jinsi kutubu kwenyewe kulivyo hasa. Wengi sana huhuzunika kwamba wametenda dhambi, na hata wanafanya matengenezo ya
nje, kwa sababu wanaogopa kwamba matendo yao mabaya waliyotenda yataleta mateso
juu yao wenyewe.
Lakini huku si kutubu kwa maana ile ya Biblia. Wao huomboleza kwa ajili ya mateso wanayopata kuliko kwa ajili ya ile dhambi waliyotenda. Hayo yalikuwa ndiyo majuto ya Esau alipoona ya kwamba alikuwa ameupoteza urithi wake milele. Balaamu, alipotiwa hofu nyingi sana kwa ajili ya kumwona malaika aliyesimama mbele yake na upanga mkononi mwake, alikiri kosa lake asije akapoteza maisha yake; lakini hakutubu kwa kweli, nia yake haikugeuka, yaani, hakuchukizwa na yale maovu,Yuda Iskariote, baada ya kumsaliti Bwana wake, alisema, “Nalikosa nilipoisaliti damu isiyo na hatia.” Mathayo 27:3.
Ungamo lile lililazimishwa kutoka katika moyo wake wenye hatia kutokana na hisia ya lawama ya kuogofya sana iliyokuwa ndani yake na kutazamia hukumu iliyokuwa mbele yake. Matokeo ambayo yangempata yalimjaza hofu kuu, lakini moyoni mwake haikuwamo huzuni yenye kina, yenye kuuvunja-vunja moyo wake, na kumwonyesha kwamba ni yeye aliyekuwa amemsaliti Mwana wa Mungu asiye na mawaa, na kumkana yule Mtakatifu wa Israeli.
Farao, alipoteswa kwa hukumu za Mungu, alikiri dhambi yake ili apate kuepuka adhabu zaidi; lakini mapigo yalipokoma, alizidi kufanya kiburi dhidi ya Mbingu. Watu hao wote waliomboleza kutokana na matokeo ya dhambi, lakini hawakuhuzunika kwa ajili ya dhambi ile yenyewe.