Lebo

01/12/2016

Kujifunza Kuomba Maombi ya Kweli

SEHEMU YA PILI.



Giza la Shetani huwafunika wale wanaoacha kuomba. Majaribu ya adui huyo anayonong’ona masikioni mwao huwashawishi wafanye dhambi; na hayo yote ni kwa sababu wao hawazitumii haki zote alizowapa Mungu katika mpango wa mbinguni wa maombi aliowawekea. Kwa nini wana na binti zake Mungu ni wazito sana kuomba,
wakati maombi ni ufunguo katika mkono wa imani uifunguao ghala ya mbinguni, ambamo zimewekwa hazina za msaada na mibaraka isiyo na mwisho ya Mungu mwenye uweza wote? Tusipoomba bila kukoma na kukesha kwa bidii, tutakuwa katika hatari ya kutojali na kukengeuka kutoka katika njia ile ya haki. Adui hutafuta daima kuzuia njia iendayo kwenye kiti cha rehema, ili kwa maombi ya dhati na imani tusiweze kupokea neema na nguvu ya kutusaidia kuyapinga majaribu.

Kuna masharti fulani ambayo yakitimizwa Mungu anaweza kutazamiwa kusikia na kujibu maombi yetu. La kwanza katika hayo ni kwamba sisi tutambue kwamba tunahitaji msaada wake. Yeye ameahidi, amesema, “Nitamimina maji juu yake aliye na kiu, na vijito vya maji juu ya mahali pakavu.” Isa. 44:3. Wale walio na njaa na kiu ya haki, wanaomtamani sana Mungu, wawe na hakika kwamba watashibishwa.
Ni lazima moyo ufunguliwe kupokea mvuto wa Roho, vinginevyo, mbaraka wa Mungu hauwezi
kupokewa. Haja yetu kuu kwa yenyewe ndiyo hoja yetu, nayo inatuombea sisi kwa ufasaha kabisa. Lakini sisi hatuna budi kumtafuta Bwana ili apate kutufanyia mambo hayo. Asema, “Ombeni, nanyi mtapewa.” Mathayo 7:7. Tena “Yeye asiyemwachilia Mwana wake mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote, atakosaje kutukirimia na mambo yote pamoja naye.” Warumi 8:32. Kama tunawaza maovu mioyoni mwetu, kama tunaing’ang’ania dhambi yoyote tuijuayo, Bwana hatatusikia; lakini sala ya mtu yule aliyetubu, na kupondeka moyo wake, inakubaliwa daima. Makosa yote tunayoyajua yanaposahihishwa, tunaweza kusadiki ya kwamba Mungu atazijibu dua zetu. Wema wetu wenyewe hauwezi kamwe kutupatia sifa za kupewa upendeleo wa Mungu; ni ustahilifu wa Yesu utakaotuokoa sisi, ni damu yake ndiyo itakayotutakasa; hata hivyo tunayo kazi ya kufanya katika
kuyatimiza masharti ya kukubaliwa naye.

Sharti jingine la maombi yanayopata ushindi ni kuwa na imani. “Pasipo imani haiwezekani kumpendeza (Mungu): kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.” Ebr. 11:6. Yesu aliwaambia wanafunzi wake, “Yoyote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu.” Marko 11:24. Je, twayasadiki maneno yake?
Ahadi hiyo ni pana, tena haina mipaka, na yule aliyeahidi ni mwaminifu. Tusipopokea mambo yale yale tuliyoyaomba kwa wakati ule ule tuombao, bado yatupasa kuamini kwamba Bwana wetu anatusikia, na ya kwamba atajibu maombi yetu. Sisi tunakosea mno, wala hatuoni mbali, hata wakati mwingine tunaomba mambo ambayo yasingekuwa mbaraka kwetu, na Baba yetu aliye mbinguni kwa upendo wake anajibu maombi yetu kwa kutupa kile ambacho kitakuwa kwa manufaa yetu ya kiwango cha juu kabisa yaani, kile ambacho sisi tungekitamani kama macho yetu yangetiwa nuru na
Mungu na tungeweza kuyaona mambo yote kama yalivyo hasa.

Maombi yetu yanapoonekana kana kwamba hayajibiwi, hatuna budi kuishikilia sana ahadi hiyo; kwa maana wakati wa kujibu utakuja hakika, nasi tutapokea mbaraka ule tunaouhitaji sana. Lakini kudai kwamba maombi yetu sikuzote yatajibiwa kwa njia ile ile hasa na ya kwamba tutapewa kitu kile kile hasa tunachokitamani ni ufidhuli. Mungu ni mwenye hekima mno hawezi kufanya kosa, tena ni mwema mno hawezi kuwanyima kitu chochote kilicho chema hao waendao kwa ukamilifu. Basi usiogope kumtegemea yeye, hata kama huoni jibu la mara moja kwa maombi yako. Tegemea ahadi yake hii ya kweli,“Ombeni, nanyi mtapewa.”

Tukishawishiwa na mashaka yetu na hofu zetu, au tukijaribu kupata ufumbuzi kwa kila kitu tusichoweza kukiona waziwazi, kabla hatujawa na imani, matatizo yetu yatazidi kuongezeka na kuwa makubwa zaidi. Lakini tukimwendea Mungu, huku tukijiona kuwa hatuna uwezo kabisa, tena tumekuwa watu wanaotegemea kusaidiwa naye, kama vile tulivyo hasa, kisha kwa unyenyekevu na imani inayomtegemea tunamjulisha, yeye ambaye maarifa yake hayana mipaka, mambo yale tunayotaka, yeye aonaye kila kitu alichokiumba, tena atawalaye vyote kwa mapenzi yake na neno lake, ndipo ataweza, tena atakisikiliza kilio chetu, na kuiangaza nuru yake mioyoni mwetu.
Kwa njia ya maombi yanayotolewa kwa moyo mnyofu tunaunganishwa na mawazo ya Mungu. Huenda tusione ushahidi wo wote wa kustaajabisha wakati uso wa Mkombozi wetu unapoinama chini na kutuangalia kwa huruma na upendo; lakini jambo hilo ndivyo lilivyo hasa. Huenda tusisikie mguso wake unaoonekana kwa macho, lakini mkono wake u juu yetu kuonyesha upendo na huruma yake inayoumia pamoja nasi.