Lebo

05/12/2015

KUUNGAMA DHAMBI__2

Wale ambao hawajajinyenyekeza mioyo yao mbele za Mungu na kuziungama dhambi zao, bado hawajalitimiza sharti la kwanza la kukubaliwa na Mungu. Kama hatujasikia toba lisilo na majuto (2 Kor. 7:10), wala hatujaziungama dhambi zetu kwa moyo wa unyenyekevu na uliovunjika, na kuyachukia maovu yetu, tutakuwa kweli hatujawahi kamwe kutafuta msamaha wa dhambi zetu; na kama hatujautafuta, basi hatujawahi kamwe kuipata amani ya Mungu. Sababu ya pekee kwa nini hatupati msamaha wa dhambi zetu zilizopita ni kwamba hatuko tayari kuinyenyekeza mioyo yetu
na kutimiza masharti ya neno la kweli.

Maagizo dhahiri yametolewa kuhusu suala hili. Ungamo la dhambi, liwe hadharani au faraghani, ni lazima litoke moyoni hasa, na litolewe kwa hiari. Mwenye dhambi asilazimishwe kutoa ungamo hilo. Wala halipaswi kutolewa kwa mzaha-mzaha tu au bila kujali, au kwa kuwalazimisha wale ambao hawana hisia yo yote juu ya hali mbaya mno ya kuchukiza ya dhambi.Ungamo lile litokalo moyoni hasa humfikia Mungu mwenye huruma isiyo na kikomo. Mtunga Zaburi asema,Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo, na waliopondeka roho huwaokoa.” Zaburi 34:18.

Ungamo la kweli daima ni la aina yake, nalo linakiri dhambi halisi zilizofanywa. Pengine ni dhambi ambazo imetupasa sisi kuzikiri kwa siri mbele za Mungu tu; pengine ni tendo baya ambalo linapaswa kuungamwa kwa mtu mmoja tu, yaani, yule aliyeathirika kutokana na tendo lile; au pengine ni kosa lililotendwa mbele ya watu lililowaumiza mioyo yao, ambalo linapaswa kuungamwa mbele yao. Lakini maungamo yote ni lazima yawe dhahiri na yakiri kosa lile lile hasa ulilolitenda.