Lebo

15/06/2016

Kumwamini Mungu na Kukubaliwa Naye 


WAKATI dhamiri yako inapokuwa imeamshwa na Roho Mtakatifu, unaona kwa kiasi fulani ubaya wa dhambi, uwezo wake, hatia yake, na jinsi iletavyo taabu, nawe unaiangalia na kuichukia kabisa.  Unaona kwamba dhambi imekutenga mbali na Mungu, kwamba wewe u mfungwa chini ya mamlaka ya dhambi.  Kadiri unavyokazana kuikwepa, ndivyo kadiri unavyotambua kwamba wewe huna nguvu kabisa.  Makusudi yako si safi;  moyo wako ni mchafu.  Unaona kwamba maisha yako yamejazwa na uchoyo na dhambi.  Unatamani sana kusamehewa, kuwekwa huru.  Kupatana na Mungu, na kufanana naye   -  je!  waweza kufanya nini ili uwe katika hali hiyo?Ni amani unayohitaji yaani, msamaha wa Mbingu na amani na upendo moyoni mwako.

Hali hii haiwezi kununuliwa kwa fedha, haipatikani kwa kutumia akili, hekima haiwezi kuipata;  kamwe huwezi kutumaini, kwa juhudi yako mwenyewe, kuipata. Lakini Mungu anakupa wewe kama zawadi, “bila fedha na bila thamani.”  Isa. 55:1, ni yako tu kama wewe utanyosha mkono wako na kuishikilia sana.  Bwana asema, “Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji;  zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu.”  Isaya 1:18. “Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu.”  Eze. 36:26. Umekwisha kuziungama  dhambi zako,  na kuziweka  mbali na  moyo wako. Umeamua kujitoa mwenyewe kwa Mungu.Basi nenda kwake, na kumwomba akusafishe dhambi zako zote, akupe moyo mpya.  Kisha amini kwamba anafanya hivyo  kwa kuwa ndivyo alivyoahidi.

Hili ndilo fundisho alilolifundisha Yesu alipokuwa hapa duniani, ya kwamba zawadi anayotuahidi Mungu kutupa, ni lazima sisi tuamini kwamba tumeipokea, nayo itakuwa yetu.Yesu aliwaponya watu maradhi yao walipouamini uwezo wake.Aliwasaidia katika mambo waliyoweza kuyaona kwa macho ya kimwili, ili wapate kumtumaini juu ya mambo wasiyoweza kuyaona, yaani, wapate kusadiki uwezo wake katika kuwasamehe dhambi zao. Hivi ndivyo alivyoeleza wazi katika kumponya yule mgonjwa aliyepooza:  “Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (amwambia yule mwenye kupooza), Ondoka, ujitwike kitanda chako, uende nyumbani  kwako.”  Mathayo 9:6.  Pia Yohana, mwinjilisti, akiongea juu ya miujiza yake Kristo, asema hivi:  “Lakini hizi zimeandikwa ili mpate kuamini ya kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu;  na kwa kuamini mwe na uzima kwa jina lake.”  Yoh. 20:31.

Kutokana na  habari za kawaida tuzipatazo katika Biblia kuhusu jinsi Yesu alivyowaponya wagonjwa, twaweza kujifunza kitu fulani juu ya kumwamini yeye kwa ajili ya msamaha wa dhambi zetu.  Hebu na tukigeukie kisa kile cha mgonjwa aliyepooza pale Bethzatha. Alikuwa hoi  kwa ugonjwa tangu miaka thelathini na minane asiweze kwenda kwa miguu. Lakini alimwamuru, alisema, “Simama, jitwike godoro lako, uende.”  Yoh. 5:8.  Yule mgonjwa angaliweza kusema:  “Bwana, kama utaniponya nitafanya usemayo.”  Lakini sivyo.  Aliliamini neno la Kristo, aliamini kwamba amepona, akajitahidi  mara moja;  akakaza  nia yake ya kwenda, naye akaenda kweli. Alifanya kama Yesu alivyosema, Mungu naye akampa nguvu, mgonjwa akapona.