VIUMBE vyote vya ulimwengu, na jinsi Mungu alivyojidhihirisha, vyote
huonyesha upendo wa Mungu. Baba yetu aliye mbinguni ndiye asili ya uhai, hekima, na
furaha. Vitazame viumbe vyote jinsi vilivyo vizuri na vya ajabu. Fikiri jinsi vifaavyo
kwa mahitaji na furaha, siyo ya wanadamu tu, bali ya viumbe vyote vilivyo hai.
Jua na mvua, huifurahisha na kuiburudisha nchi, pamoja na vilima, bahari na mabonde, vyote
hutuonyesha upendo wa Muumbaji wetu. Mungu ndiye anayevipatia viumbe vyake
vyote mahitaji yao ya kila siku. Katika maneno mazuri ya Mtunga Zaburi twasoma haya,
“Macho ya watu wote yakuelekea Wewe;
Nawe huwapa chakula chao kwa wakati wake.
Waufumbua mkono wako,Wakishibisha kilicho hai matakwa yake.
”Zaburi 145:15,16.
Mungu alimwumba mwanadamu katika hali ya furaha na utakatifu kamili; na
wakati nchi ilipotoka mkononi mwa Muumba, ilikuwa nzuri kabisa; haikuwa na dalili ya
uharibifu wala laana ya Mungu. Taabu na mauti viliingia kwa sababu ya kuivunja sheria
ya Mungu sheria ya upendo. Lakini, hata katikati ya maumivu yatokanayo na dhambi,
upendo wa Mungu umedhihirishwa. Imeandikwa ya kwamba Mungu aliilaani ardhi kwa
ajili ya mwanadamu. Mwanzo 3:17.
Miti yenye miiba na magugu - yaani, shida na majaribu yanayoyafanya maisha yake kuwa ya taabu na wasiwasi - yaliwekwa kwa manufaa yake, ili yawe sehemu mojawapo ya mafundisho yake yanayotakiwa katika mpango wa Mungu, ili apate kumtoa katika hali mbaya ya dhambi na kumrudisha katika hali njema aliyokuwa nayo mara ya kwanza.