Lebo

Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo UTUME. Onyesha machapisho yote
Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo UTUME. Onyesha machapisho yote

02/12/2016

Kujifunza Kuomba Maombi ya Kweli

SEHEMU YA TATU.


Tunapomwendea Mungu kumwomba rehema zake na mbaraka wake, ingetupasa kuwa na roho ya upendo ndani ya mioyo yetu wenyewe. Twawezaje kuomba hivi, “Utusamehe deni zetu, kama sisi nasi tuwasamehevyo wadeni wetu,” wakati sisi katika roho zetu tungali hatujakubali kuwasamehe wengine. Tukitumaini kujibiwa maombi yetu, sharti tuwe na roho ya kuwasamehe wengine kwa njia ile ile, na kwa kiwango kile kile, kama sisi tunavyotarajia kusamehewa.

Kudumu katika maombi ni sharti jingine lililowekwa ili tupate kupokea.Yatupasa kuomba sikuzote, kama tunataka kukua katika imani na katika uzoefu wa maisha yetu. “Katika kusali, mkidumu,” “dumuni sana katika kuomba, mkikesha katika kuomba huku na shukrani.” Rum. 12:12; Kol. 4:2. Petro awausia Wakristo, “Iweni na akili, mkeshe katika sala.” 1 Petro 4:7. Mtume Paulo awaagiza hivi, “Katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane kwa Mungu.” Flp.4:6. Na Yuda pia asema, “Ninyi, wapenzi, mkijijenga juu ya imani yenu iliyo takatifu
sana, na kuomba katika Roho Mtakatifu, jilindeni katika upendo wa Mungu.” Yuda 20,21. Kuomba bila kukoma ni muungano wa mtu na Mungu usioweza kuvunjika, kiasi kwamba uhai toka kwa Mungu unabubujika na kuingia katika maisha yetu; na kutoka katika maisha yetu usafi wa maisha na utakatifu hububujika na kumrudia Mungu.

Umuhimu upo wa kufanya bidii katika kuomba; usikubali kitu cho chote kikuzuie kuomba fanya kila jitihada kuacha wazi mawasiliano kati ya roho yako na Yesu tafuta kila nafasi kwenda mahali ambapo watu huzoea kuomba wale wanaotaka kushirikiana na Mungu kweli kweli wataonekana kila mara kwenye mkutano wa maombi; watakuwa waaminifu katika kufanya wajibu wao, tena watakuwa na bidii na shauku katika kujipatia manufaa yote wawezayo kupata. Watatumia vizuri kila nafasi wapatayo ili kujiweka mahali wawezapo kupokea mionzi ya nuru kutoka mbinguni.

Sharti tuombe pamoja na watu wa nyumbani; na zaidi ya yote tusiwe wavivu katika kuomba faraghani peke yetu; maana kufanya hivyo ndiyo asili ya uzima wa roho zetu. Ni vigumu kabisa kusitawi kiroho wakati maombi yanapuuzwa. Maombi pamoja na watu wa nyumbani na yale ya watu wengi katika ibada hayatoshi. Hebu mahali pale pa faragha moyo wako na ufunguliwe wazi ili upate kuchunguzwa na jicho lake Mungu.
Maombi ya faragha ya mtu akiwa peke yake yanapaswa kusikilizwa tu na Mungu asikiaye maombi. Hakuna sikio lo lote lenye udadisi linalopaswa kupokea mzigo wa dua kama hizo. Katika maombi hayo ya siri mtu hasumbuliwi na mivuto inayomzunguka, hasumbuliwi na misisimko yo yote. Kwa utulivu, lakini kwa dhati, moyo wake unamtafuta Mungu. Mvuto utokao kwake yeye aonaye sirini, ambaye sikio lake li wazi kusikiliza maombi yatokayo moyoni, utakuwa mtamu na wa kudumu. Kwa imani tulivu, ya kawaida, mtu huyo anaongea na Mungu, na kujikusanyia mionzi ya nuru itokayo kwa Mungu inayomtia nguvu na kumtegemeza katika mapambano yake na Shetani. Mungu ni mnara wa nguvu zetu. Omba katika chumba chako cha siri; na unapokwenda kufanya kazi zako za kila siku, umwinulie Mungu moyo wako mara kwa mara. Hivyo ndivyo Henoko alivyopata kutembea pamoja na Mungu. Maombi hayo ya kimya kimya hupanda juu kama uvumba wa thamani kwenda mbele ya kiti cha neema. Shetani hawezi kamwe kumshinda yule ambaye moyo wake humtegemea Mungu hivyo.

Hakuna wakati wala mahali pasipofaa kumwomba Mungu. Hakuna kinachoweza kutuzuia tusimwinulie mioyo yetu tukiwa na roho ya maombi ya dhati. Tukiwa katika makundi ya watu mitaani, katikati ya shughuli zetu za kazi, tunaweza kupeleka dua zetu kwa Mungu, na kumwomba atupe uongozi wake, kama alivyoifanya Nehemia alipotoa ombi lake mbele ya Mfalme Artashasta. Chumba cha siri cha mawasiliano kinaweza kupatikana po pote tulipo. Mlango wa moyo wetu ungefunguliwa wazi daima, na mwaliko wetu ungepanda juu ili Yesu aje na kukaa ndani ya moyo wetu kama mgeni atokaye mbinguni.

01/12/2016

Kujifunza Kuomba Maombi ya Kweli

SEHEMU YA PILI.



Giza la Shetani huwafunika wale wanaoacha kuomba. Majaribu ya adui huyo anayonong’ona masikioni mwao huwashawishi wafanye dhambi; na hayo yote ni kwa sababu wao hawazitumii haki zote alizowapa Mungu katika mpango wa mbinguni wa maombi aliowawekea. Kwa nini wana na binti zake Mungu ni wazito sana kuomba,
wakati maombi ni ufunguo katika mkono wa imani uifunguao ghala ya mbinguni, ambamo zimewekwa hazina za msaada na mibaraka isiyo na mwisho ya Mungu mwenye uweza wote? Tusipoomba bila kukoma na kukesha kwa bidii, tutakuwa katika hatari ya kutojali na kukengeuka kutoka katika njia ile ya haki. Adui hutafuta daima kuzuia njia iendayo kwenye kiti cha rehema, ili kwa maombi ya dhati na imani tusiweze kupokea neema na nguvu ya kutusaidia kuyapinga majaribu.

Kuna masharti fulani ambayo yakitimizwa Mungu anaweza kutazamiwa kusikia na kujibu maombi yetu. La kwanza katika hayo ni kwamba sisi tutambue kwamba tunahitaji msaada wake. Yeye ameahidi, amesema, “Nitamimina maji juu yake aliye na kiu, na vijito vya maji juu ya mahali pakavu.” Isa. 44:3. Wale walio na njaa na kiu ya haki, wanaomtamani sana Mungu, wawe na hakika kwamba watashibishwa.
Ni lazima moyo ufunguliwe kupokea mvuto wa Roho, vinginevyo, mbaraka wa Mungu hauwezi
kupokewa. Haja yetu kuu kwa yenyewe ndiyo hoja yetu, nayo inatuombea sisi kwa ufasaha kabisa. Lakini sisi hatuna budi kumtafuta Bwana ili apate kutufanyia mambo hayo. Asema, “Ombeni, nanyi mtapewa.” Mathayo 7:7. Tena “Yeye asiyemwachilia Mwana wake mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote, atakosaje kutukirimia na mambo yote pamoja naye.” Warumi 8:32. Kama tunawaza maovu mioyoni mwetu, kama tunaing’ang’ania dhambi yoyote tuijuayo, Bwana hatatusikia; lakini sala ya mtu yule aliyetubu, na kupondeka moyo wake, inakubaliwa daima. Makosa yote tunayoyajua yanaposahihishwa, tunaweza kusadiki ya kwamba Mungu atazijibu dua zetu. Wema wetu wenyewe hauwezi kamwe kutupatia sifa za kupewa upendeleo wa Mungu; ni ustahilifu wa Yesu utakaotuokoa sisi, ni damu yake ndiyo itakayotutakasa; hata hivyo tunayo kazi ya kufanya katika
kuyatimiza masharti ya kukubaliwa naye.

Sharti jingine la maombi yanayopata ushindi ni kuwa na imani. “Pasipo imani haiwezekani kumpendeza (Mungu): kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.” Ebr. 11:6. Yesu aliwaambia wanafunzi wake, “Yoyote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu.” Marko 11:24. Je, twayasadiki maneno yake?
Ahadi hiyo ni pana, tena haina mipaka, na yule aliyeahidi ni mwaminifu. Tusipopokea mambo yale yale tuliyoyaomba kwa wakati ule ule tuombao, bado yatupasa kuamini kwamba Bwana wetu anatusikia, na ya kwamba atajibu maombi yetu. Sisi tunakosea mno, wala hatuoni mbali, hata wakati mwingine tunaomba mambo ambayo yasingekuwa mbaraka kwetu, na Baba yetu aliye mbinguni kwa upendo wake anajibu maombi yetu kwa kutupa kile ambacho kitakuwa kwa manufaa yetu ya kiwango cha juu kabisa yaani, kile ambacho sisi tungekitamani kama macho yetu yangetiwa nuru na
Mungu na tungeweza kuyaona mambo yote kama yalivyo hasa.

Maombi yetu yanapoonekana kana kwamba hayajibiwi, hatuna budi kuishikilia sana ahadi hiyo; kwa maana wakati wa kujibu utakuja hakika, nasi tutapokea mbaraka ule tunaouhitaji sana. Lakini kudai kwamba maombi yetu sikuzote yatajibiwa kwa njia ile ile hasa na ya kwamba tutapewa kitu kile kile hasa tunachokitamani ni ufidhuli. Mungu ni mwenye hekima mno hawezi kufanya kosa, tena ni mwema mno hawezi kuwanyima kitu chochote kilicho chema hao waendao kwa ukamilifu. Basi usiogope kumtegemea yeye, hata kama huoni jibu la mara moja kwa maombi yako. Tegemea ahadi yake hii ya kweli,“Ombeni, nanyi mtapewa.”

Tukishawishiwa na mashaka yetu na hofu zetu, au tukijaribu kupata ufumbuzi kwa kila kitu tusichoweza kukiona waziwazi, kabla hatujawa na imani, matatizo yetu yatazidi kuongezeka na kuwa makubwa zaidi. Lakini tukimwendea Mungu, huku tukijiona kuwa hatuna uwezo kabisa, tena tumekuwa watu wanaotegemea kusaidiwa naye, kama vile tulivyo hasa, kisha kwa unyenyekevu na imani inayomtegemea tunamjulisha, yeye ambaye maarifa yake hayana mipaka, mambo yale tunayotaka, yeye aonaye kila kitu alichokiumba, tena atawalaye vyote kwa mapenzi yake na neno lake, ndipo ataweza, tena atakisikiliza kilio chetu, na kuiangaza nuru yake mioyoni mwetu.
Kwa njia ya maombi yanayotolewa kwa moyo mnyofu tunaunganishwa na mawazo ya Mungu. Huenda tusione ushahidi wo wote wa kustaajabisha wakati uso wa Mkombozi wetu unapoinama chini na kutuangalia kwa huruma na upendo; lakini jambo hilo ndivyo lilivyo hasa. Huenda tusisikie mguso wake unaoonekana kwa macho, lakini mkono wake u juu yetu kuonyesha upendo na huruma yake inayoumia pamoja nasi.

29/11/2016

Kujifunza Kuomba Maombi ya Kweli

SEHEMU YA KWANZA



MUNGU huzungumza nasi kupitia katika viumbe vyake vya asili na mafunuo yake, kupitia katika maongozi yake, na kwa njia ya Roho wake. Lakini njia hizo hazitoshi; sisi pia tunahitaji kumfungulia mioyo yetu. Ili tupate uzima wa kiroho na nguvu yake, hatuna budi kuongea na Baba yetu aliye mbinguni. Mawazo yetu yanaweza kuvutwa kwake; tunaweza kuzitafakari kazi zake, rehema zake, baraka zake; lakini hayo, kwa maana yake kamili, si kuongea naye. Ili tuweze kuongea na Mungu, ni sharti tuwe na mambo fulani ya kumwambia hasa kuhusu maisha yetu tunayoishi.Katika kuomba tunamfunulia Mungu mioyo yetu na kuongea naye kama tunavyoongea na rafiki wa kweli. Si lazima kufanya hivyo ili kumjulisha Mungu hali yetu ilivyo, bali kuongea naye kunatuwezesha kumpokea mioyoni mwetu.

Maombi hayamlazimishi Mungu kushuka kwetu, bali ni sisi ambao tunainuliwa mpaka kufika
kwake. Yesu alipokuwapo hapa duniani, aliwafundisha wanafunzi wake kusali. Aliwaagiza waweke mahitaji yao ya kila siku mbele za Mungu, na kumtwika mizigo yao yote. Na ahadi ile aliyowapa kwamba dua zao zingesikilizwa ni ahadi iliyotolewa kwetu pia. Yesu mwenyewe, alipokaa na wanadamu, aliomba mara nyingi.
Mwokozi wetu alishiriki katika shida zetu na udhaifu wetu; hivyo akawa mhitaji na mwombaji, akimwomba Baba yake ili apate nguvu mpya za kufanya kazi yake na kuwa tayari kupambana na kazi na majaribu yatakayompata. Yeye ndiye mfano wetu katika mambo yote. Ni ndugu yetu ashirikiye udhaifu wetu, “alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote;” lakini kwa sababu alikuwa hana dhambi, aliyaepuka maovu nafsini mwake; alistahimili mapambano na maumivu makali moyoni mwake katika dunia hii yenye dhambi. Ubinadamu wake ulifanya maombi kuwa ya lazima kwake na haki yake.

Alipata faraja na furaha katika kuongea na Baba yake. Na iwapo Mwokozi huyo wa wanadamu, Mwana wa Mungu, aliona kwamba anahitaji kuomba, je! sisi, tulio wanadamu dhaifu wenye dhambi, tusingeona kwamba ni jambo la lazima zaidi kwetu kuomba bila kukoma. Baba yetu aliye mbinguni anangojea kutumwagia baraka zake juu yetu kwa utimilifu. Ni fursa yetu kunywa maji mengi kwenye chemchemi ya pendo lake.
Ni jambo la kushangaza jinsi gani ya kwamba sisi tunaomba kidogo mno! Mungu yu tayari, tena
anapenda kusikiliza maombi ya kweli ya mtoto wake aliye duni kabisa, walakini sisi kwa upande wetu hatuna moyo sana wa kumwambia Mungu haja zetu. Hivi malaika wa mbinguni wanafikirije kuhusu wanadamu maskini wasio na msaada wo wote, ambao wanakabiliwa na majaribu, wakati moyo wa Mungu uliojaa upendo usio na kikomo unapowaonea shauku nyingi sana, akiwa tayari kuwapa zaidi ya yale waombayo au kufikiria, na bado maombi yao ni kidogo sana, tena wana imani ndogo kabisa? Malaika wanapenda kusujudu mbele zake Mungu; wanapenda kuwa karibu naye. Wanaona kwamba maongezi yao na Mungu ni upeo wa furaha yao; lakini watoto wa dunia hii,
wanaohitaji msaada mwingi mno ambao ni Mungu pekee awezaye kuwapa, wanaonekana
kana kwamba wametosheka kutembea bila ya kuwa na nuru ya Roho wake, yaani, ushirika wa kuwako kwake.

Giza la Shetani huwafunika wale wanaoacha kuomba. Majaribu ya adui huyo anayonong’ona masikioni mwao huwashawishi wafanye dhambi; na hayo yote ni kwa sababu wao hawazitumii haki zote alizowapa Mungu katika mpango wa mbinguni wa maombi aliowawekea. Kwa nini wana na binti zake Mungu ni wazito sana kuomba, wakati maombi ni ufunguo katika mkono wa imani uifunguao ghala ya mbinguni, ambamo zimewekwa hazina za msaada na mibaraka isiyo na mwisho ya Mungu mwenye uweza wote? Tusipoomba bila kukoma na kukesha kwa bidii, tutakuwa katika hatari ya kutojali na kukengeuka kutoka katika njia ile ya haki. Adui hutafuta daima kuzuia njia iendayo kwenye kiti cha rehema, ili kwa maombi ya dhati na imani tusiweze kupokea
neema na nguvu ya kutusaidia kuyapinga majaribu.

28/09/2016

KAZI NA MAISHA.................

SOMO LA TATU


Kanisa lake Kristo ni njia aliyoiweka Mungu kwa ajili ya wokovu wa wanadamu. Kazi yake ni kueneza Injili duniani kote. Na wajibu huo umewekwa juu ya Wakristo wote. Kila mmoja, kulingana na kiwango cha talanta yake na nafasi nzuri anayopewa, anapaswa kutimiza agizo hilo la Mwokozi. Upendo wa Kristo, uliofunuliwa kwetu, unatufanya sisi kuwa wadeni kwa wote wasiomjua. Mungu ametupa nuru, si kwa ajili yetu wenyewe, bali kwa ajili ya kuiangaza juu yao. Wafuasi wa Kristo kama wangeamka na kufanya wajibu wao, kungekuwako na watu elfu wa kuhubiri Injili mahali palipo na mhubiri mmoja tu sasa katika nchi za kipagani.
Na wale ambao wasingeweza kujiingiza wenyewe kufanya kazi hiyo bado wangeweza kuisaidia kwa kutoa fedha zao, kuiunga mkono, na kwa maombi yao. Tena pangekuwa na juhudi kubwa zaidi katika kazi ya kuongoa roho katika nchi za Kikristo. Hatuna haja ya kwenda katika nchi za kipagani au hata kuondoka na kwenda nje ya mduara mdogo wa nyumba zetu, kama kazi yetu ipo pale, ili kuweza kumtumikia Kristo. Tunaweza kufanya kazi hiyo katika mduara wa nyumbani mwetu, katika kanisa,
miongoni mwa wale tunaoshirikiana nao, na miongoni mwa wale tunaofanya nao kazi au
biashara.

Sehemu kubwa sana ya maisha ya Mwokozi wetu hapa duniani ilitumika kwa kufanya kazi ngumu katika kiwanda cha seremala kule Nazareti. Malaika wahudumuo waliandamana naye huyo Bwana wa uzima alipotembea pamoja na wakulima wadogo na vibarua, bila ya kutambulikana wala kupewa heshima. Kwa uaminifu alikuwa akitimiza utume wake alipokuwa akifanya kazi yake ile duni sawasawa na wakati ule alipowaponya wagonjwa au kutembea juu ya mawimbi ya Galilaya yenye kurushwa huku na huku kwa dhoruba. Kwa hiyo, katika kazi zetu duni kabisa na vyeo vyetu vya chini kabisa katika maisha yetu tunaweza kutembea na kufanya kazi pamoja na Yesu.
Mtume Paulo asema, “Kila mtu na akae katika hali iyo hiyo aliyoitwa mbele za Mungu.” 1 Kor. 7:24. Mfanya biashara anaweza kufanya kazi yake kwa namna ambavyo anaweza kumtukuza Mungu kwa uaminifu wake. Kama yeye ni mfuasi wa kweli wa Kristo, basi, ataonyesha dini yake katika kila kitu afanyacho, na kuwadhihirishia watu roho ya Kristo. Fundi mitambo anaweza kuwa mwakilishi mwenye bidii na mwaminifu wa yule aliyefanya kazi ya sulubu katika hali duni ya maisha kati ya
vilima vya Galilaya. Kila mtu anayelitaja jina lake Kristo angefanya kazi kwa namna ambayo wengine, wakiyaona matendo yake mema, wavutwe na wamtukuze Muumbaji na Mkombozi wao.

Wengi wametoa udhuru ili wasivitumie vipawa vyao katika kumtumikia Kristo kwa sababu wengine wanavyo vipawa bora sana na hali yao ni nzuri sana. Wazo limeenea kote kwamba ni wale tu walio na talanta za pekee ndio wanatakiwa kutumia uwezo wao katika kumtumikia Mungu. Imekuja kuelewekwa na wengi kwamba talanta zinatolewa kwa kundi fulani tu lililopendelewa, na kuwaacha wengine, ambao, kwa kweli, hawatakiwi kushiriki katika kazi hizo ngumu au katika thawabu zake. Lakini haijaelezwa hivyo katika mfano huu. Bwana wa nyumba alipowaita watumishi wake,
alimpa kazi “kila mtu kwa kadiri ya uwezo wake.” Mt. 25:15. Tukiwa na moyo wa upendo tunaweza kufanya kazi duni kabisa za maisha “kama kwa Bwana.” Kol. 3:23. Upendo wa Mungu ukiwamo moyoni, utaonekana katika maisha yetu. Harufu nzuri ya Kristo itatuzunguka pande zote, na mvuto wetu utawainua watu na kuwaletea furaha.
Haikupasi kungojea matukio makubwa au kutarajia kuwa na uwezo wa ajabu kabla hujaenda kufanya kazi ya Mungu. Huna haja ya kuwaza ulimwengu utakuonaje wewe. Kama maisha yako ya kila siku yanashuhudia usafi wa maisha yako na unyofu wa imani yako, na wengine wameamini kwamba unataka kuwanufaisha wao, basi, juhudi zako hazitapotea kamwe. Wafuasi wa Yesu walio duni na maskini kabisa wanaweza kuwa mbaraka kwa wengine. Huenda wao wasitambue kwamba wanafanya jema lo lote maalumu, lakini kwa mvuto wao usiotambulikana wanaweza kuanzisha mawimbi ya mibaraka yatakayozidi kupanuka na kuwa na kina kirefu, na matokeo yake yenye mibaraka huenda wasiweze kamwe kuyajua mpaka siku ile ya mwisho ya kupewa thawabu zao. Wao
hawajisikii au hawajui kwamba wanafanya kitu cho chote kikubwa. Hawatakiwi kujichosha wenyewe kwa kuingiwa na wasiwasi juu ya mafanikio. Wao wanapaswa tu kusonga mbele kimya kimya, wakifanya kwa uaminifu kazi ile ambayo Mungu amewapa kufanya, na maisha yao hayatakuwa bure. Roho zao zitakuwa zikikua zaidi na zaidi na kufanana na Kristo; wao ni watenda kazi pamoja na Kristo katika maisha haya, na kwa njia hiyo wanajitayarisha kwa kazi ile ya juu zaidi na furaha isiyokuwa na huzuni ya maisha yale yajayo.

27/09/2016

KAZI NA MAISHA ..............

SOMO LA PILI


Tukijitahidi hivyo kusaidia wengine, sisi pia tutabarikiwa. Hili lilikuwa ndilo kusudi la Mungu alipotupa sisi sehemu ya kufanya katika mpango wake wa ukombozi. Amewapa wanadamu fursa ya kuwa washirika wa tabia ya uungu, nao, kwa upande wao, wanapaswa kuitawanya mibaraka hiyo kwa wanadamu wenzao. Hiyo ni heshima ya juu kabisa, hiyo ni furaha ipitayo zote, ambayo inawezekana kwa Mungu kuwapa wanadamu. Wale wanaoshiriki hivyo katika kazi hiyo ya upendo wanaletwa karibu sana na Muumbaji wao.
Mungu angaliweza kuwapa malaika wa mbinguni ujumbe wa Injili, pamoja na kazi yote ya kutoa huduma ya upendo kwa wanadamu. Angaliweza kuzitumia njia nyingine katika kulitimiza kusudi lake. Lakini katika upendo wake usio na kikomo alichagua kutufanya sisi kuwa watenda kazi pamoja naye, yaani, pamoja na Kristo na malaika zake, ili tupate kushiriki katika mbaraka na furaha hiyo, na kutiwa moyo kiroho, mambo ambayo ni matokeo ya huduma hiyo isiyo na ubinafsi. Tunakuwa na moyo ule ule wa huruma aliokuwa nao Kristo tunaposhiriki mateso yake. Kila tendo la kujinyima kwa manufaa ya wengine huimarisha roho ya ukarimu katika moyo wa mtoaji, na kumfanya afungamane kwa karibu zaidi na Mkombozi wa ulimwengu, ambaye “alikuwa tajiri, lakini kwa ajili yenu akawa maskini, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake.” 2 Kor. 8:9, Na ni wakati ule tu tunapolitimiza kusudi la Mungu la kutuumba sisi, ndipo maisha yanaweza kuwa mbaraka kwetu.

Endapo utafanya kazi kama Kristo alivyokusudia wafuasi wake wafanye, na kuongoa roho za watu kwa ajili yake, utaona haja ya kuwa na uzoefu wa maisha wenye kina zaidi na ujuzi mkubwa zaidi katika mambo ya Mungu, tena utaona njaa na kiu ya kuitafuta haki yake. Utamsihi sana Mungu, na imani yako itaimarishwa, na nafsi yako itakunywa maji mengi katika kisima cha wokovu. Kupambana na upinzani na maonjo kutakufanya uikimbilie Biblia na maombi. Utakua katika neema na katika kumjua Kristo, nawe utakuwa na uzoefu wa thamani.
Roho ya kuwatumikia wengine bila ya kuwa na ubinafsi inaifanya tabia iwe na kina, thabiti, tena iwe na upendo wa Kristo, inaleta amani na furaha kwa yule aliye nayo. Hamu ya kupata mambo yaliyo bora huongezeka. Hakuna nafasi kwa uvivu, wala uchoyo. Wale wanaojizoeza hivyo kutumia hisani zao za Kikristo watakua kiroho, tena watakuwa na nguvu katika kufanya kazi ya Mungu. Watakuwa na utambuzi safi wa kiroho, na imani thabiti inayozidi kukua, na uwezo ulioongezeka katika maombi yao. Roho wa Mungu, anapoigusa mioyo yao, anataka pawe na amani takatifu moyoni, kama
jibu la mguso huo wa Mungu. Wale wanaoutumia muda wao wote kutenda kazi hiyo bila
ya kuwa na ubinafsi kwa ajili ya manufaa ya wengine wanafanya kazi ya kuziokoa roho zao wenyewe kwa hakika kabisa.

Njia pekee ya kukua katika neema ni ile ya kufanya kazi ile ile aliyotuagiza Kristo kuifanya  pasipo kujifikiria wenyewe, kwa uwezo wetu wote, kuwasaidia na kuwaletea furaha wale wanaohitaji msaada wetu tuwezao kuwapa. Nguvu zinakuja kwa kufanya mazoezi; kujishughulisha ndilo sharti hasa la kuwa na uzima. Wale wanaojitahidi kudumisha maisha yao ya Kikristo kwa kupokea mibaraka inayowajia kwa njia ya neema pasipo kujishughulisha, wala kufanya kazi yo yote kwa ajili ya Kristo, wanajaribu tu kuishi kwa kuendelea kula bila kufanya kazi. Na katika ulimwengu wa
kiroho kama ilivyo katika ulimwengu wa asili, matokeo yake sikuzote ni uharibifu na
uozo. Mtu ambaye angekataa kufanya mazoezi ya viungo vyake angepoteza uwezo wote wa kuvitumia baada ya muda mfupi. Hivyo Mkristo ambaye hazitumii nguvu zake alizopewa na Mungu siyo tu kwamba anashindwa kukua katika Kristo, bali anapoteza
nguvu alizokuwa nazo tayari.

26/09/2016

KAZI NA MAISHA........

SOMO LA KWANZA


MUNGU ndiye asili ya uhai na mwanga na furaha kwa malimwengu yote. Kama mionzi ya nuru kutoka juani, kama vijito vya maji kutoka kwenye chemchemi hai, baraka zinamiminika kutoka kwake kwenda kwa viumbe vyake vyote. Na kila mahali ambapo uhai wa Mungu umo ndani ya mioyo ya wanadamu, utabubujika kuwa upendo na mbaraka kwa wengine.
Ilikuwa ni furaha ya Mwokozi wetu kuwainua na kuwakomboa wanadamu walioanguka dhambini. Kwa ajili hiyo hakuyahesabu maisha yake kuwa ni kitu cha thamani kwake, lakini “aliustahimili msalaba na kuidharau aibu.” Ebr. 12:2. Kwa ajili hiyo malaika wanashughulika daima katika kazi ya kuwaletea wengine furaha. Hiyo ndiyo furaha yao. Ile ambayo watu wale wajipendao binafsi wangeiona kuwa ni kazi ya kuwavunjia heshima, yaani, kuwahudumia wale walio na hali mbaya na ambao kwa kila hali ni duni kwa tabia na hadhi zao, ndiyo kazi waifanyayo malaika wasio na dhambi.Roho aliyo nayo Kristo ya upendo unaojitoa mhanga ndiyo roho iliyoenea kule mbinguni,
na ndiyo msingi hasa wa furaha kuu iliyoko kule. Hiyo ndiyo roho watakayokuwa nayo
wafuasi wake Kristo, ndiyo kazi watakayofanya.

Upendo wa Kristo ukiwamo moyoni, kama manukato yenye harufu nzuri, hauwezi kufichika. Mvuto wake mtakatifu utawagusa wote tunaokutana nao. Roho ya Kristo ikiwamo moyoni ni kama chemchemi jangwani, inayobubujika na kuwaburudisha wengi, na kuwafanya wale walio tayari kuangamia kutamani kunywa maji ya uzima. Kuwa na upendo kwa Yesu kutadhihirika kwa njia ya kuwa na tamaa ya kutenda kama alivyotenda yeye, kwa madhumuni ya kuwaletea furaha na kuwatia moyo wanadamu. Kutaleta upendo, upole, na huruma kwa viumbe vyote vya Baba yetu aliye mbinguni anayevitunza.
Maisha ya Mwokozi wetu alipokuwa hapa duniani hayakuwa maisha ya raha, wala ya kujishughulikia mwenyewe tu, lakini daima alijitahidi kufanya kazi kwa bidii, bila kuchoka kwa ajili ya wokovu wa wanadamu waliopotea. Tangu kuzaliwa kwake mpaka kusulibiwa kwake pale Kalwari, alifuata njia ya kujinyima, wala hakutaka aachiliwe asifanye kazi za sulubu, safari zenye kumletea maumivu, na shughuli kwa watu zinazochosha mno na kazi za kawaida. Alisema, “Kama vile Mwana wa Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.”
Mathayo 20:28. Hilo lilikuwa ndilo lengo moja kuu la maisha yake. Mambo mengine yote yalichukua nafasi ya pili na kulisaidia lengo hilo. Kilikuwa ni chakula na kinywaji chake kufanya mapenzi ya Mungu na kuimaliza kazi yake (Yoh. 4:34). Nafsi na umimi havikuwa na nafasi katika kazi yake.

Kwa hiyo wale wanaoshiriki neema ya Kristo watakuwa tayari kujinyima sana, ili wengine aliowafia wapate karama hiyo. Watafanya kila wawezalo kuifanya dunia hii iwe mahali pazuri kwa ajili ya kukaa kwao hapa. Roho hii ni matokeo ya hakika ya kukua kiroho kwa mtu yule aliyeongoka kweli kweli. Mara tu anapokuja kwa Kristo, ndani yake hujitokeza shauku ya kuwajulisha wengine jinsi alivyomwona Yesu kuwa rafiki wa thamani sana kwake; kweli ile iokoayo na kutakasa haiwezi kufungiwa moyoni mwake. Kama tumevikwa haki ya Kristo, na kujazwa furaha ya Roho wake akaaye ndani yetu hatutaweza kunyamaza. Kama tumeonja na kuona kwamba Bwana ni mwema, tutakuwa na jambo fulani la kusimulia. Kama Filipo alivyomwona Mwokozi, tutawaalika wengine
kuja mbele yake. Tutajitahidi kuweka mbele yao mambo ya kuvutia pamoja na mambo yale ya kweli ya ulimwengu ule ujao ili waje kwa Kristo. Tutakuwa na shauku kubwa kuifuata njia ile aliyokwenda Yesu. Tutatamani kwa dhati sana kwamba wale watuzungukao waweze kumwona “Mwana-Kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu.” Yoh. 1:29