SOMO LA TATU
Kanisa lake Kristo ni njia aliyoiweka Mungu kwa ajili ya wokovu wa wanadamu. Kazi yake ni kueneza Injili duniani kote. Na wajibu huo umewekwa juu ya Wakristo wote. Kila mmoja, kulingana na kiwango cha talanta yake na nafasi nzuri anayopewa, anapaswa kutimiza agizo hilo la Mwokozi. Upendo wa Kristo, uliofunuliwa kwetu, unatufanya sisi kuwa wadeni kwa wote wasiomjua. Mungu ametupa nuru, si kwa ajili yetu wenyewe, bali kwa ajili ya kuiangaza juu yao. Wafuasi wa Kristo kama wangeamka na kufanya wajibu wao, kungekuwako na watu elfu wa kuhubiri Injili mahali palipo na mhubiri mmoja tu sasa katika nchi za kipagani.
Na wale ambao wasingeweza kujiingiza wenyewe kufanya kazi hiyo bado wangeweza kuisaidia kwa kutoa fedha zao, kuiunga mkono, na kwa maombi yao. Tena pangekuwa na juhudi kubwa zaidi katika kazi ya kuongoa roho katika nchi za Kikristo. Hatuna haja ya kwenda katika nchi za kipagani au hata kuondoka na kwenda nje ya mduara mdogo wa nyumba zetu, kama kazi yetu ipo pale, ili kuweza kumtumikia Kristo. Tunaweza kufanya kazi hiyo katika mduara wa nyumbani mwetu, katika kanisa,
miongoni mwa wale tunaoshirikiana nao, na miongoni mwa wale tunaofanya nao kazi au
biashara.
Sehemu kubwa sana ya maisha ya Mwokozi wetu hapa duniani ilitumika kwa kufanya kazi ngumu katika kiwanda cha seremala kule Nazareti. Malaika wahudumuo waliandamana naye huyo Bwana wa uzima alipotembea pamoja na wakulima wadogo na vibarua, bila ya kutambulikana wala kupewa heshima. Kwa uaminifu alikuwa akitimiza utume wake alipokuwa akifanya kazi yake ile duni sawasawa na wakati ule alipowaponya wagonjwa au kutembea juu ya mawimbi ya Galilaya yenye kurushwa huku na huku kwa dhoruba. Kwa hiyo, katika kazi zetu duni kabisa na vyeo vyetu vya chini kabisa katika maisha yetu tunaweza kutembea na kufanya kazi pamoja na Yesu.
Mtume Paulo asema, “Kila mtu na akae katika hali iyo hiyo aliyoitwa mbele za Mungu.” 1 Kor. 7:24. Mfanya biashara anaweza kufanya kazi yake kwa namna ambavyo anaweza kumtukuza Mungu kwa uaminifu wake. Kama yeye ni mfuasi wa kweli wa Kristo, basi, ataonyesha dini yake katika kila kitu afanyacho, na kuwadhihirishia watu roho ya Kristo. Fundi mitambo anaweza kuwa mwakilishi mwenye bidii na mwaminifu wa yule aliyefanya kazi ya sulubu katika hali duni ya maisha kati ya
vilima vya Galilaya. Kila mtu anayelitaja jina lake Kristo angefanya kazi kwa namna ambayo wengine, wakiyaona matendo yake mema, wavutwe na wamtukuze Muumbaji na Mkombozi wao.
Wengi wametoa udhuru ili wasivitumie vipawa vyao katika kumtumikia Kristo kwa sababu wengine wanavyo vipawa bora sana na hali yao ni nzuri sana. Wazo limeenea kote kwamba ni wale tu walio na talanta za pekee ndio wanatakiwa kutumia uwezo wao katika kumtumikia Mungu. Imekuja kuelewekwa na wengi kwamba talanta zinatolewa kwa kundi fulani tu lililopendelewa, na kuwaacha wengine, ambao, kwa kweli, hawatakiwi kushiriki katika kazi hizo ngumu au katika thawabu zake. Lakini haijaelezwa hivyo katika mfano huu. Bwana wa nyumba alipowaita watumishi wake,
alimpa kazi “kila mtu kwa kadiri ya uwezo wake.” Mt. 25:15. Tukiwa na moyo wa upendo tunaweza kufanya kazi duni kabisa za maisha “kama kwa Bwana.” Kol. 3:23. Upendo wa Mungu ukiwamo moyoni, utaonekana katika maisha yetu. Harufu nzuri ya Kristo itatuzunguka pande zote, na mvuto wetu utawainua watu na kuwaletea furaha.
Haikupasi kungojea matukio makubwa au kutarajia kuwa na uwezo wa ajabu kabla hujaenda kufanya kazi ya Mungu. Huna haja ya kuwaza ulimwengu utakuonaje wewe. Kama maisha yako ya kila siku yanashuhudia usafi wa maisha yako na unyofu wa imani yako, na wengine wameamini kwamba unataka kuwanufaisha wao, basi, juhudi zako hazitapotea kamwe. Wafuasi wa Yesu walio duni na maskini kabisa wanaweza kuwa mbaraka kwa wengine. Huenda wao wasitambue kwamba wanafanya jema lo lote maalumu, lakini kwa mvuto wao usiotambulikana wanaweza kuanzisha mawimbi ya mibaraka yatakayozidi kupanuka na kuwa na kina kirefu, na matokeo yake yenye mibaraka huenda wasiweze kamwe kuyajua mpaka siku ile ya mwisho ya kupewa thawabu zao. Wao
hawajisikii au hawajui kwamba wanafanya kitu cho chote kikubwa. Hawatakiwi kujichosha wenyewe kwa kuingiwa na wasiwasi juu ya mafanikio. Wao wanapaswa tu kusonga mbele kimya kimya, wakifanya kwa uaminifu kazi ile ambayo Mungu amewapa kufanya, na maisha yao hayatakuwa bure. Roho zao zitakuwa zikikua zaidi na zaidi na kufanana na Kristo; wao ni watenda kazi pamoja na Kristo katika maisha haya, na kwa njia hiyo wanajitayarisha kwa kazi ile ya juu zaidi na furaha isiyokuwa na huzuni ya maisha yale yajayo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Tuandikie maoni yako hapa. Leave your comments here