Lebo

28/11/2016

KUMJUA MUNGU

SOMO LA PILI.
                                                             

Jambo kuu la ukombozi ni moja ambalo malaika wanatamani kulichungulia; litakuwa ndiyo sayansi na wimbo wa waliokombolewa milele hata milele. Je, si jambo lifaalo kufikiriwa sana na kuchunguzwa nasi katika siku hizi? Rehema isiyo na kikomo na upendo wa Yesu, kafara iliyotolewa kwa ajili yetu, mambo hayo hututaka sisi tuyatafakari kwa makini na kwa uzito wake.

Tungeongelea sana juu ya tabia ya Mpendwa Mkombozi na Mwombezi wetu. Tungetafakari sana juu ya utume wake yeye aliyekuja kuwaokoa watu wake kutoka katika dhambi zao. Tukitafakari hivyo juu ya mambo makuu ya mbinguni, imani yetu na upendo wetu vitakua na kuwa na nguvu nyingi zaidi, na maombi yetu yatazidi kukubalika na Mungu, kwa sababu yatakuwa yamechanganyika na imani na upendo kwa wingi zaidi. Yatatolewa kwa akili na kwa dhati. Na tunapowaza mambo matakatifu, imani yetu itaongezeka kwake, na upendo wetu pia, tena kwa ajili hiyo maombi yetu yatazidi kukubaliwa na Mungu. Kuwa na imani na

Yesu kutazidi kuongezeka daima, pamoja na uzoefu hai wa maisha ya kila siku unaoutegemea uweza wake wa “kuwaokoa kabisa wale wote wamjiao Mungu kwa yeye.” Waeb. 7:25. Na tunapotafakari juu ya ukamilifu alio nao Mwokozi, tutatamani kugeuzwa tabia zetu kabisa, na kufanywa upya kufanana naye katika usafi wake. Patakuwa na njaa na kiu ya roho ya kutaka kufanana naye yule tumpendaye sana. Kadiri tunavyozidi kumfikiria zaidi Kristo, ndivyo kadiri tutakavyozidi kuongea habari zake kwa wengine na kumwakilisha ulimwenguni.
Biblia haikuandikwa kwa ajili ya wataalamu wa Biblia peke yao; kinyume chake, ilitayarishwa kwa ajili ya watu wa kawaida. Kweli zile kuu ambazo ni za lazima kwa wokovu zimeelezwa waziwazi kama nuru ya adhuhuri; wala hakuna mtu ye yote awezaye kukosa kuzielewa na kupotea njia isipokuwa ni wale wanaofuata maoni yao wenyewe badala ya mapenzi ya Mungu yaliyofunuliwa wazi.

Tusikubali kupokea ushuhuda wa mtu ye yote juu ya kile Maandiko yafundishacho, ila tujifunze sisi wenyewe maneno hayo ya Mungu. Tukiwaruhusu wengine kufikiri mambo ya Biblia kwa niaba yetu, tutakuwa na nguvu kama ya kiwete na uwezo uliopungua sana nguvu yake. Nguvu bora za akili zetu zinaweza kudumaa mno kwa kukosa mazoezi ya kufikiri juu ya mambo makuu yanayofaa kutafakariwa kiasi cha kuweza kupoteza uwezo wake wa kuelewa maana zenye kina za Neno la Mungu.
Ubongo wetu utapanuka ukitumika kuchunguza uhusiano uliopo kati ya masomo ya Biblia, Maandiko yakilinganishwa na Maandiko, na mambo ya kiroho yakilinganishwa
na mambo ya kiroho.Hakuna njia nyingine iliyokusudiwa kuitia akili nguvu nyingi zaidi kama ile ya
kujifunza na kuyachunguza Maandiko. Hakuna kitabu kingine kilicho na uwezo mkubwa mno wa kuyakuza mawazo yetu, kuzipa nguvu fahamu za ubongo wetu, kama zilivyo hizo kweli pana, ziadilishazo, za Biblia. Kama wanadamu wangejifunza na kulichunguza Neno la Mungu kama inavyostahili, wangekuwa na maarifa mengi na tabia bora, na kuwa na kusudi thabiti ambalo katika nyakati hizi ni shida mno kuliona.
Lakini kuna manufaa kidogo tu yanayopatikana kwa kusoma Maandiko kwa haraka. Mmoja anaweza kuisoma Biblia yote, lakini bado ashindwe kutambua uzuri wake, wala kuelewa maana yake yenye kina iliyojificha. Kujifunza kifungu kimoja cha maneno mpaka maana yake imekuwa dhahiri, na uhusiano wake na mpango wa wokovu unaeleweka wazi, kuna manufaa mengi sana kuliko kuzisoma sura nyingi kwa juu juu tu bila ya kuwa na kusudi lo lote dhahiri wala kupata mafundisho yo yote yanayojenga.

Biblia yako iwe karibu nawe kila mara. Kila upatapo nafasi, isome; jifunze mafungu yake kwa moyo. Hata wakati utembeapo mitaani, waweza kusoma fungu fulani, na kwa njia hiyo kulikaza mawazoni mwako.Hatuwezi kupata hekima bila kujitahidi kwa dhati na kujifunza kwa moyo wa maombi. Baadhi ya sehemu za Maandiko maana yake imekuwa dhahiri kabisa; lakini kuna sehemu nyingine ambazo maana yake si rahisi kufahamika mara moja. Maandiko yanapaswa kulinganishwa na Maandiko mengine. Lazima pawe na utafiti wa makini na kutafakari kwa moyo wa maombi. Na kujifunza kama huko kutapata malipo maradufu. Kama vile mchimba madini anavyogundua mabamba ya mawe ya madini ya thamani yaliyojificha chini ya uso wa nchi, ndivyo yule anayestahimili kulichunguza Neno la Mungu, kama hazina iliyositirika, azionavyo kweli za thamani kuu mno, ambazo zimefichwa asiweze kuziona mtafutaji mzembe. Maneno hayo ya uvuvio, tukiyatafakari mioyoni mwetu, yatakuwa kama vijito vitiririkavyo kutoka katika chemchemi ya uzima.