SOMO LA TATU.
Tusifungue kabisa Biblia na kuyasoma maneno yake bila kuomba. Kabla ya kuzifungua kurasa zake ingetupasa kuomba ufahamu kutoka kwa Roho Mtakatifu, naye atatupa. Nathanaeli alipomwendea Yesu, Mwokozi alisema, “Tazama, Mwisraeli kweli kweli, hamna hila ndani yake.” Nathanaeli akamwambia, “Umepataje kunitambua?”Yesu akajibu, akamwambia, “Kabla Filipo hajakuita, ulipokuwapo chini ya mtini, nilikuona.” Yoh. 1:47,48. Na Yesu atatuona sisi mahali pa siri pa sala, ikiwa tutamwomba ili tupate kuelimishwa na kuyajua yaliyo ya kweli.
Malaika watokao kwenye ulimwengu ule wa nuru watakuwa pamoja na wale ambao kwa unyenyekevu wa moyo wanatafuta uongozi wa Mungu. Roho Mtakatifu humwinua na kumtukuza Mwokozi. Ni kazi yake kutuonyesha Kristo, na hali yake jinsi ilivyo yenye haki na usafi, na kutudhihirishia habari za wokovu mkuu tupatao kwake. Yesu alisema, “Atatwaa katika yaliyo yangu, na kuwapasha habari.” Yohana 16:14. Roho wa kweli ndiye mwalimu pekee awezaye kutujulisha
barabara ile kweli ya Mungu. Ni dhahiri kwamba Mungu huwaona wanadamu kuwa wa thamani kubwa, kwa kuwa alimtoa Mwanawe afe kwa ajili yao, tena amemweka Roho
wake kuwa mwalimu na kiongozi wa wanadamu daima.
Nataka nimjue Yesu,
Na nizidi kumfahamu;
Nijue pendo lake tu,
Wokovu wake kamili.
Nataka nione Yesu,
Na nizidi kusikia
Anenapo kitabuni,
Kujidhihirisha kwangu.
Nataka tena zaidi,
Daima kupambanua
Mapenzi yake, nifanye
Yale yanayompendeza.
Nataka nikae naye,
Kwa mazungumzo matamu.
Nizidi kuwaonyesha
Wengine wokovu wake.
Zaidi, zaidi,
Nimfahamu Yesu,
Nijue upendo wake,
Wokovu wake kamili.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Tuandikie maoni yako hapa. Leave your comments here