SOMO LA PILI.
Yesu hufundisha jambo lile lile asemapo, “Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu, kadhalika nanyi, msipokaa ndani yangu…. Maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lolote.” Yoh. 15:4,5.
Wewe unamtegemea Kristo ili kuishi maisha matakatifu sawasawa na tawi linavyofungamana na mti wenyewe ili lipate kukua na kuzaa matunda. Pasipo yeye huna uzima. Huna nguvu ya kuyapinga majaribu au ya kukuwezesha kukua katika neema na utakatifu. Ukikaa ndani yake, waweza kusitawi. Ukipata uzima kutoka kwake huwezi kunyauka wala kukosa kuzaa matunda. Utakuwa kama mti uliopandwa kando ya mito yenye maji.
Wengi hudhani kwamba ni wajibu wao kufanya sehemu ya kazi ile wenyewe wamemtumainia Kristo kwa msamaha wa dhambi zao, lakini sasa wanaona ya kwamba kwa juhudi zao wenyewe wanaweza kuishi maisha yaliyo safi. Lakini kila juhudi ya aina hiyo ni lazima ishindwe. Yesu asema, “Pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lolote.” Kukua kwetu katika neema, furaha yetu, kuwa na manufaa kwetu kwa wengine mambo hayo yote hutegemea muungano wetu na Kristo. Ni kwa njia ya kuongea naye, kila siku, kila saa tunapaswa kukua katika neema.
Yeye siye tu mwenye kuianzisha imani yetu, bali ndiye mwenye kuitimiza. Kristo ndiye wa kwanza na wa mwisho na wa sikuzote. Anakuwa pamoja nasi, si mwanzo tu na mwisho wa njia yetu, bali katika kila hatua tunayotembea katika njia hiyo. Daudi asema, “Nimemweka Bwana mbele yangu
daima, kwa kuwa yuko kuumeni kwangu, sitaondoshwa.” Zaburi 16:8. Pengine unauliza, “Nawezaje kukaa ndani ya Kristo?” Kama ulivyompokea moyoni mara ya kwanza. “Kama mlivyompokea Kristo Yesu, Bwana, enendeni vivyo hivyo katika yeye.” “Mwenye haki ataishi kwa imani.” Kol. 2:6; Ebr. 10:38. Ulijitoa kwa Mungu kuwa mtu wake kabisa, kumtumikia na kumtii, tena ulimpokea Kristo kama Mwokozi wako.
Wewe mwenyewe hukuweza kujiondolea dhambi zako, wala kuugeuza moyo wako; lakini ulipokuwa umejitoa kuwa wa Mungu, ndipo uliposadiki kwamba Mungu ndiye aliyekutendea haya yote kwa ajili ya Kristo. Kwa njia ya imani ulikuwa wake Kristo; na kwa imani hiyo utazidi kukua ndani yake - kwa kujitoa na kumpokea. Yakupasa kutoa vyote kwake - moyo wako, nia yako, na utumishi wako - jitoe kwake ili upate kuyatii matakwa yake yote; tena yakupasa kupokea vyote – Kristo, utimilifu wa
baraka zote, ili akae moyoni mwako, awe nguvu zako, haki yako, na msaidizi wako
daima - ili akupe nguvu za kukuwezesha kumtii.
Jitoe kwake Mungu kila asubuhi, kabla hujafanya kitu cho chote. Omba hivi: “Bwana wangu, unichukue, niwe wako kamili. Mipango yangu yote naiweka miguuni pako. Unitumie leo katika kazi yako. Ukae nami, ili kazi yangu yote itendeke katika wewe.” Hili ndilo jambo lipaswalo kufanywa kila siku. Kila asubuhi ujitoe kuwa wa Mungu kwa siku ile. Weka mipango yako yote mbele yake, ili kuifanya au kutoifanya kama atakavyokuonyesha. Hivyo ndivyo siku kwa siku waweza kuendelea kuyakabidhi maisha yako mkononi mwa Mungu, na maisha yako yatafanana zaidi na zaidi na maisha
yake Kristo.
Maisha ndani ya Kristo ni maisha ya raha mustarehe. Huenda pasiwepo na hisia ya furaha kuu moyoni mwako, lakini patakuwa na matumaini yenye utulivu unaodumu. Matumaini yako hayamo ndani yako mwenyewe; yamo ndani ya Kristo. Udhaifu wako unaunganishwa na nguvu zake, kutojua kwako huunganishwa na hekima yake, unyonge wako unaunganishwa na uwezo wake udumuo daima. Hivyo haifai kuiangalia nafsi yako mwenyewe, kuyaacha mawazo yako kuwaza juu ya nafsi yako; bali mwangalie Kristo tu.
Fikiri sana juu ya upendo wake, juu ya uzuri na utimilifu wa tabia yake. Kristo alivyojinyima, Kristo alivyojidhili, Kristo alivyokuwa na maisha safi na matakatifu,Kristo katika upendo wake usio na kifani, hayo ndiyo mambo yafaayo kufikiriwa moyoni. Ni kwa njia ya kumpenda yeye, kumwiga matendo yake na tabia yake, kumtegemea kabisa, ndipo utaweza kugeuka kabisa na kufanana naye.
Yesu asema, “Kaeni ndani yangu.” Maneno haya yanatupa wazo la kukaa mustarehe na kuwa imara, na kuwa na matumaini. Asema tena, “Njoni kwangu,… nami nitawapumzisha.” Mathayo 11:28. Maneno haya ya Mtunga Zaburi yanaeleza wazo lilo hilo: “Ukae kimya mbele za Bwana, nawe umngojee kwa saburi.” Zab. 37:7. Naye Isaya anatuhakikishia hivi: “Nguvu zenu zitakuwa katika kutulia na kutumaini.” Isaya 30:15. Kustarehe huku hakupatikani kwa kukaa bure katika hali ya kutofanya kazi; maana katika mwaliko wa Mwokozi ahadi ya kupata raha imefungamana na wito wa kufanya kazi. “Jitieni nira yangu,… nanyi mtapata raha.” Mathayo 11:29. Yule anayemtegemea
Kristo kabisa atakuwa mtu mwenye moyo na juhudi nyingi kabisa katika kumtumikia
Mungu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Tuandikie maoni yako hapa. Leave your comments here