AFICHAYE dhambi zake hatafanikiwa; bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema.” Mithali 28:13.
Masharti yanayompasa mtu kufanya ili apate rehema ya Mungu si magumu, ni ya
haki na ya maana. Bwana hataki tufanye jambo fulani zito ili tupate kusamehewa dhambi
zetu. Hatuna haja ya kufanya hija ndefu na za kuchosha kwenda mahali patakatifu, wala
kujipiga-piga kuonyesha toba yetu, ili Mungu wa mbinguni apendezwe nasi, ama kufanya
malipo kwa ajili ya makosa yetu; lakini yeye aziungamaye dhambi zake na kuziacha,
ndiye atakayesamehewa.
Mtume Yakobo asema, “Ungameni dhambi zenu (kigiriki, makosa yenu) ninyi kwa ninyi, na kuombeana, mpate kuponywa.” Yak. 5:16. Ungama dhambi zako kwa Mungu ambaye ndiye peke yake awezaye kuzisamehe, na makosa yako uliyowatendea wengine uyaungame mbele yao. Endapo umemfanyia rafiki au jirani yako kosa lililomchukiza, unapaswa kuliungama kosa lako kwake, naye ni wajibu wake kukusamehe kabisa.
Kisha yakupasa kuomba msamaha kwa Mungu, kwa sababu huyo mwenzako ni kiumbe cha Mungu, na kumfanyia mwanadamu makosa ni kumfanyia makosa Muumba na Mwokozi wake. Jambo hilo linawekwa mbele ya Mpatanishi pekee wa kweli, Kuhani wetu Mkuu, ambaye “alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi,” na ambaye aweza “kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu,” na awezaye kutusafisha uchafu wote wa dhambi. Ebr. 4:15.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Tuandikie maoni yako hapa. Leave your comments here