Lebo

07/12/2015

KUUNGAMA DHAMBI__3

Zamani wakati wa Samweli, Waisraeli walimwasi Mungu. Walikuwa wakiteseka kama matokeo ya dhambi zao; maana walikuwa wamepoteza imani yao kwa Mungu, walikuwa wamepoteza utambuzi wao kuhusu nguvu na hekima yake katika kulitawala taifa lile, walipoteza imani yao kuhusu uwezo wake wa kuwalinda na kuithibitisha kazi yake.

Wakampa kisogo Mfalme Mkuu wa Malimwengu, na kutamani kutawaliwa kama mataifa yale yaliyowazunguka. Kabla hawajaipata amani, walitoa ungamo hili halisi: “Tumeongeza dhambi zetu kwa uovu huu, wa kujitakia mfalme.” 1 Sam. 12:19. Kosa lile lile hasa ambalo walitiwa hatiani lilipaswa kuungamwa. Kutokuwa na shukrani kwao kuliitesa mioyo yao, na kuwatenga mbali na Mungu.

Ungamo halitakubaliwa na Mungu bila ya kuwapo toba ya kweli na badiliko la maisha. Lazima badiliko dhahiri lionekane katika maisha ya mtu; kila kitu kimchukizacho Mungu ni lazima kiondolewe na kutupwa mbali. Hayo yatakuwa ndiyo matokeo ya huzuni ya kweli kwa ajili ya dhambi. Kazi ile tupaswayo kufanya kwa upande wetu imewekwa wazi mbele yetu: “Jiosheni, jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu usiwe mbele za macho yangu; acheni kutenda mabaya; jifunzeni kutenda mema;takeni hukumu na haki; wasaidieni walioonewa; mpatieni yatima haki yake; mteteeni mjane.”

 Isa. 1:16,17. “Kama mtu mwovu akirudisha rehani, na kumrudishia mtu mali yake aliyomnyang’anya, akizifuata sheria za uzima, asitende uovu wo wote; hakika ataishi, hatakufa.” Eze. 33:15. Paulo, akiongea juu ya kazi ya toba, asema hivi: “Maana angalieni, kuhuzunishwa kuko huko kwa jinsi ya Mungu kulitenda bidii kama nini ndani yenu; naam, na kujitetea, naam, na kukasirika, naam, na hofu, naam, na shauku, naam, na kujitahidi, naam, na kisasi! Kwa kila njia mmejionyesha wenyewe kuwa safi katika jambo hilo.” 2 Kor. 7:11.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Tuandikie maoni yako hapa. Leave your comments here