Lebo

12/12/2015

KUUNGAMA DHAMBI__4

Dhambi inapozifisha hisia za kiroho, mwenye dhambi hatambui kasoro alizo nazo katika tabia yake, wala hatambui ukubwa wa dhambi aliyoitenda; na kama hajisalimishi chini ya uwezo umhakikishiao dhambi wa Roho Mtakatifu, anabaki katika hali ya kuwa nusu kipofu kwa dhambi yake. Maungamo yake si ya kweli wala hayatolewi kwa dhati.

Kwa kila kosa analoungama anaongeza kutoa udhuru kwa ajili ya njia yake mbaya huku akijipongeza, akisema kwamba laiti mambo yasingalikuwa vile, asingekuwa amefanya kosa hili au lile, ambalo kwalo anakaripiwa.

Adamu na Hawa walipokwisha kula matunda yaliyokatazwa, walijaa haya na hofu kuu. Kwanza kabisa, walifikiri namna ya kujitetea kwa ajili ya kosa lao, ili waepukane na hukumu ya kifo waliyoiogopa sana. Bwana alipowauliza habari ya kosa lao, Adamu alijibu, huku kwa sehemu fulani akiliweka kosa lile juu ya Mungu na kwa sehemu juu ya mwenzi wake: “Mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala.” Yule mwanamke akamtupia lawama nyoka, akasema, “Nyoka alinidanganya, nikala.” Mwanzo 3:12,13. Kwa nini ulimwumba nyoka? Kwanini ulimruhusu aje katika Edeni? Haya ndiyo maswali yaliyojificha katika udhuru aliotoa kwa ajili ya dhambi yake, kwa njia hiyo akimshitaki Mungu kuwa anawajibika kwa anguko lao.

Roho ya kujihesabia haki mtu mwenyewe mwanzo wake ilitoka kwa yule baba wa uongo, nayo imedhihirishwa na wana na binti wote wa Adamu. Maungamo ya jinsi hii hayavuviwi na Roho wa Mungu, wala hayatakubaliwa na Mungu. Ungamo la kweli litamfanya mtu abebe dhambi yake mwenyewe, na kuiungama bila ya kuwa na udanganyifu au unafiki. Kama yule mtoza ushuru maskini, pasipo kuinua sana macho yake kuelekea mbinguni, atalia, akisema, “Mungu uniwie radhi mimi mwenye dhambi;” na wale wanaokiri dhambi zao watahesabiwa haki; kwa maana Yesu atawaombea akidai damu yake iliyomwagika kwa ajili ya mwenye dhambi atubuye.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Tuandikie maoni yako hapa. Leave your comments here