Lebo

16/05/2016

KILE ANACHOTAKA MUNGU

Wakati huu Mungu anataka kile kile alichotaka kwa watakatifu wale wawili kule Edeni utii kamili kwa matakwa yake. Sheria yake [Amri Kumi] inaendelea kuwa ni ile ile kwa vizazi vyote. Kanuni [kipimo] kuu ya haki iliyotolewa katika Agano la Kale haijapunguzwa katika Agano Jipya. Si kazi ya Injili kupunguza nguvu ya madai ya Sheria takatifu ya Mungu [Amri Kumi] ila kuwainua wanadamu juu ili wawe mahali wanapoweza kuzishika amri zake [kumi]. Imani katika Kristo inayomwokoa mwanadamu si kama vile inavyohubiriwa na wengi. "Amini, amini," ndicho kilio chao; "mwamini tu Kristo, nawe utaokoka. Hayo ndiyo yote unayopaswa kufanya." Wakati imani ya kweli inamtegemea Kristo kabisa kwa wokovu, itamwongoza [yule aliye nayo] kwenye utii kamili kwa Sheria ya Mungu [Amri Kumi]. Imani inadhihirishwa kwa matendo.
Tena, yule mtume Yohana anatangaza, akisema, "Yeye asemaye, Nimemjua [Nimeokoka], wala hazishiki amri zake [kumi], ni mwongo, wala kweli haimo ndani yake" (1 Yohana 2:4). Si salama kutegemea hisia [kujisikia moyoni] au misisimko; mambo hayo ni viongozi wasioweza kutegemewa. Sheria ya Mungu [Amri Kumi] ndiyo kanuni ya utakatifu peke yake.
 Ni kwa njia ya Sheria hiyo [Amri Kumi] tabia ya mtu itapimwa. Kama mtu ye yote anayeulizia wokovu angeuliza swali hili, "Nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?" waalimu wa siku hizi wanaofundisha utakaso wangejibu hivi, "Amini tu kwamba Yesu anakuokoa." Lakini Yesu alipoulizwa swali hilo alimwambia, "Imeandikwa nini katika torati? Wasomaje? Yule aliyeuliza swali hilo akamjibu, akisema, "Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote,... na jirani yako kama nafsi yako," Yesu akamwambia, "Umejibu vema; fanya hivi nawe utaishi" (Luka 10:25-29).Utakaso wa kweli utashuhudiwa kwa heshima ile anayoionyesha mtu kwa bidii na kwa uaminifu wake kwa amri zote [kumi] za Mungu, kwa uangalifu wake katika kuikuza kila talanta aliyopewa, kwa maongezi yake yenye busara, na kwa kuonyesha katika kila tendo analotenda upole ule wa Kristo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Tuandikie maoni yako hapa. Leave your comments here