Kwa njia nyingi Mungu anajaribu kutujulisha tabia yake, ili tupate kumjua na kushirikiana naye. Viumbe vya asili huongea na akili zetu pasipo kukoma. Moyo unaofunguliwa wazi utaguswa na upendo na utukufu wa Mungu kama unavyoonekana katika matendo yake na katika kazi za mikono yake. Sikio lisikilizalo laweza kusikia na kuelewa ujumbe wa Mungu kupitia katika vitu hivyo vya asili. Mashamba ya kijani kibichi, miti mirefu sana, chipukizi na maua, wingu lipitalo, mvua inyeshayo, kijito kibubujikacho, utukufu wa huko mbinguni, huongea na mioyo yetu, na kutualika sisi ili tufahamiane na yeye aliyeviumba hivyo vyote.
Mwokozi wetu aliyafungamanisha, pamoja na vitu hivyo vya asili, mafundisho yake ya thamani. Miti, ndege, maua ya mabondeni, vilima, maziwa, na mbingu zinazopendeza, pamoja na matukio na mazingira ya maisha yetu ya kila siku, yote yalifungamanishwa na maneno yake ya kweli, ili mafundisho yake yapate kukumbukwa kwa njia hiyo, hata katikati ya shughuli nyingi za maisha ya taabu ya mwanadamu.
Mungu angependa watoto wake wapendezwe na kazi zake, na kufurahia uzuri wa kawaida, uliofichika, ambao kwa huo ameipamba nyumba yetu ya kidunia. Yeye ni mpenzi wa vitu vizuri, na kupita hivyo vyote ambavyo kwa nje hupendeza na kuvutia, yeye anaipenda tabia nzuri; angependa sisi tukuze usafi wa maisha na kuwa na maisha ya kawaida tu, yaani tabia zilizofichika kama zile za maua.Kama tutasikiliza tu, basi, viumbe vilivyoumbwa na Mungu vitatufundisha mafundisho ya thamani juu ya utii na kumtegemea yeye. Kuanzia na nyota ambazo zinafuata njia zao zisizo na alama katika anga za juu na kizazi kwa kizazi zinafuata njia yao ziliyowekewa, mpaka chini kwenye atomu ndogo kabisa, viumbe vya asili huyatii mapenzi ya Muumbaji. Tena Mungu hukitunza na kukilisha kila kitu alichokiumba.
Yule anayeyashikilia malimwengu yasiyohesabika katika eneo kubwa sana, wakati uo huo anajali mahitaji ya shomoro mdogo wa kikahawia aimbaye wimbo wake mdogo pasipo hofu.Wanadamu wanapoondoka asubuhi kwenda kazini, na wakati waombapo; wakati wanapokwenda kulala usiku; na wakati wanapoamka asubuhi; tajiri anapofanya karamu katika jumba lake, au maskini anapowakusanya watoto wake kukizunguka chakula chao kidogo, kila mmoja huangaliwa kwa huruma na upendo na Baba yetu aliye mbinguni.Hakuna chozi limtokalo mtu ambalo Mungu halioni. Hakuna tabasamu yo yote asiyoiona. Kama tungesadiki hivyo kabisa, mahangaiko yote yasiyofaa yangeondolewa mioyoni mwetu. Maisha yetu yasingejazwa na kukata tamaa mno kama yalivyo sasa; kwa sababu kila kitu, kiwe kikubwa au kidogo, kingeachwa mikononi mwake Mungu,
ambaye hachanganyikiwi kuona ongezeko kubwa la masumbufu yetu, wala halemewi na mizigo yake. Hapo ndipo tungeweza kuifurahia amani mioyoni mwetu ambayo kwa wengi kwa muda mrefu imekuwa kitu kigeni.
Akili yako inapoufurahia uzuri uvutiao wa dunia hii, hebu fikiria ulimwengu ule ujao, ambao haujui kamwe waa la dhambi wala kifo; ambao ndani yake uso wa maumbile hautakuwa na kivuli cha laana tena. Hebu mawazo yako na yapige picha na kuyaona makao ya waliookolewa, kisha kumbuka kwamba yatakuwa na utukufu mwingi sana kuliko mawazo yako makali sana yawezavyo kuiona picha ile. Katika zawadi mbalimbali alizotupa katika maumbile tunaona tu nuru hafifu mno ya utukufu wake. Imeandikwa, “Mambo ambayo jicho halikuyaona wala sikio halikuyasikia, wala
hayakuingia katika moyo wa mwanadamu, mambo ambayo Mungu aliwaandalia
wampendao.” 1 Kor. 2:9.
Mtunga mashairi pamoja na mwanasayansi anayeshughulika na viumbe vya asili wanayo mambo mengi ya kusema juu ya maumbile, lakini ni Mkristo anayeufurahia uzuri wa dunia hii kwa shukrani kubwa mno, kwa sababu anatambua kazi ya mikono ya Baba yake, na kuuona upendo wake katika ua na kichaka na mti. Hakuna mtu ye yote awezaye kutambua kwa ukamilifu umuhimu wa kuwapo kilima na bonde, mto na bahari, ambaye havioni vitu hivyo kuwa ni ufunuo wa upendo wa Mungu alio nao kwa mwanadamu.
Mungu husema nasi katika matendo yake na uongozi wake, tena katika mvuto wa Roho wake mioyoni mwetu. Katika mambo yanayotokea kwetu, na katika mazingira yetu, katika mabadiliko yanayotokea kila siku pande zote, twaweza kupata mafundisho ya thamani, kama mioyo yetu imekuwa wazi kuyatambua mafundisho hayo. Mtunga Zaburi, akifuatilia matendo na uongozi wa Mungu, asema hivi, “Nchi imejaa fadhili za Bwana.” “Aliye na hekima na ayaangalie hayo, na wazitafakari fadhili za Bwana.” Zaburi 33:5; 107:43. Mungu husema nasi katika Neno lake. Humo imefunuliwa dhahiri sana tabia yake, jinsi anavyowatendea wanadamu, na kazi yake kubwa ya ukombozi. Humo zimesimuliwa habari za wazee wakuu na manabii na watakatifu wengine wa zamani. Walikuwa ni watu wenye “tabia moja na sisi.” Yakobo 5:17. Tunaona jinsi walivyopambana na mambo ya kukatisha tamaa kama yale tuliyo nayo sisi, jinsi walivyoanguka majaribuni kama sisi tulivyoanguka; hata hivyo walijitia moyo tena, wakashinda kwa neema ya Mungu; na sisi tukiwaangalia, tunatiwa moyo katika jitihada yetu ya kupata haki. Tunaposoma habari za mambo makuu waliyoyapitia katika maisha yao, habari za nuru na upendo na baraka waliyofurahiwa nayo, na habari za kazi waliyoifanya kwa neema ya Mungu, ndipo roho ile iliyowaongoza wao inawasha mwako mtakatifu na tamaa mioyoni mwetu, na kutupa hamu ya kufanana nao katika tabia – kuwa
kama wao katika kutembea na Mungu.
Yesu alisema hivi kuhusu Maandiko ya Agano la Kale - na je! si zaidi sana kwamba yale ya Jipya ni ya kweli - “hayo ndiyo yanayonishuhudia,” yaani, yanamshuhudia Mkombozi wetu, ambaye ndani yake matumaini yetu ya uzima wa milele yamewekwa. Yoh. 5:39. Naam, Biblia nzima inasimulia habari za Kristo. Tangu habari za mwanzo juu ya kuumbwa kwa ulimwengu, - kwa kuwa “pasipo yeye hakikufanyika chochote kilichofanyika,” Yoh. 1:3, mpaka ahadi ya mwisho, “Tazama, naja upesi,” Ufu. 22:12, twasoma juu ya matendo yake, tena twaisikiliza sauti yake. Kama unataka
kumjua Mwokozi, jifunze Maandiko Matakatifu. Ujaze moyo wako wote maneno ya Mungu. Hayo ndiyo maji ya uzima, yanakata kiu yako. Hayo ndiyo mkate wa uzima utokao mbinguni. Yesu asema, “Msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu.” Akazidi kueleza maana yake hivi: “Maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima.” Yoh.
6:53,63. Miili yetu imejengwa kutokana na chakula tulacho na kinywaji tunywacho; na
kama ilivyo katika vitu vya asili, ndivyo ilivyo katika mambo ya kiroho: ni kile tunachokitafakari sana kitakachotupa afya na nguvu katika tabia yetu ya kiroho.